Stewart alivyopokewa Uwanja wa Ndege jana. Picha kwa hisani ya straikamkali.blogspot.com |
Na Mahmoud Zubeiry
LEO NI LEO
kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar
es Salaam, ambako timu mbili zinazopigana vikumbo katika nafasi ya tatu,
wenyeji Azam FC watamenyana na Coastal Union ya Tanga katika mfululizo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hiyo ni moja
kati ya mechi tamu za Ligi Kuu, zisizozihusisha Simba na Yanga, kwani ukiondoa
wababe hao wa soka Tanzania, kama kuna timu nyingine inayoweza kufikiriwa japo
kushika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo, ni kati ya hizo, Azam na Coastal.
Azam imekuwa
katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu kwa muda mrefu, kabla ya kushushwa hadi
nafasi ya nne ndani ya siku mbili mwishoni mwa wiki na Coastal ndio ya tatu
sasa, nyuma ya Yanga na Simba, zinazolinganana kwa pointi.
Coastal
inayofundishwa na kocha mtaalamu, lakini ‘simpo tu’, Ahmed Morocco itamenyana
na Azam leo ambayo itaongozwa na Kali Ongala, anayekaimu Ukocha Mkuu, kufuatia
kufukuzwa kwa Mserbia, Boris Bunjak Jumatatu.
Baada ya
kufukuzwa kwa Bunjak, Azam imekwishamrejesha kocha wake wa zamani, Muingereza
Stewart Hall ambaye alitua jana usiku na leo atakuwapo Chamazi.
Bunjak
ameondoka Azam baada ya kuiongoza timu katika mechi 16, akifungwa nne tu, zote
dhidi ya Simba ikiwemo ya juzi ya Ligi Kuu, waliyofungwa 3-1 na kutoa sare
tatu.
Bunjak
mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), alitua Azam, Agosti 7, mwaka
huu akitokea FC Damac ya Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na
kabla ya hapo alifundisha klabu kibao za kwao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK
Javor Ivanjica, Crvena Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK
Mladi Radnik, FK Crvena Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
Awali,
Bunjak aliyezaliwa Novemba 17, mwaka 1954 ( miaka 57), alicheza soka katika
klabu za FK Sloga (Kraljevo), FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki (Kragujevac),
FK Olimpia (Ljubljana), FK Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo), FK
Borac (Cacak) na FK Sloga (Kraljevo).
Stewart
alifukuzwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo,
kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Mserbia huyo
anakuwa kocha wa tano kufukuzwa Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza
Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na
Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini
Stewart angalau aliacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha
kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu
Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi
uliopita, mambo ambayo bila shaka yamemfanya afikiriwe tena.
Stewart ana
sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano
namna ambavyo alikuwa akimpromoti Kali Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji,
lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono, akashauriana naye awe Kocha Msaidizi
na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, akakubali.
Chini ya
Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na
mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali,
ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika
90.
Yote kwa
tote, Chamazi leo kinachotarajiwa ni soka safi, ile ya burudani, isiyokuwa na
presha kutokana na timu hizo kutokuwa na mashabiki wenye ugonjwa wa moyo kama
wale wa Simba na Yanga.
Wakati huo
huo: Stewart Hall alitua jana usiku mjini Dar es Salaam na kusema anataka Azam ishinde
kila mechi kuanzia sasa baada ya kurejea kazini.
Hall
amerejea katika klabu yake ya zamani ya Azam baada klabu aliyokuwa akiifundisha
Sofapaka ya Kenya inayomilikiwa na tajiri kukiri kwamba haiwezi kupambana na
kampuni kubwa ya Azam ambayo imeahidi kumpa mshahara mara mbili ya waliokuwa
wakimlipa Wakenya hao.
Mashabiki
waliokuwa uwanjani hapo wakipuliza mavuvuzela na kupiga ngoma, waliimba nyimbo
mbalimbali ukiwamo uliosema "Hall amerejea, homa na presha za Simba na
Yanga ziko juu."
Baada ya
kutua kocha huyo, alivishwa mataji ya maua na viongozi wa Azam waliokuwapo
kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumpokea.