Mshambuliaji wa Tanzania John Bocco akichezewa kindava na mabeki wa Burundi mbele ya refa Ronnie Kalema wa Uganda. |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
BAO pekee la
mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Suleiman Ndikumana dakika ya 52, leo
limeizamisha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika mchezo wa Kundi B, Kombe
la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge Uwanja wa Mandela,
Namboole, usiku huu.
Nahodha huyo
wa Burundi, anayechezea Inter Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, alifunga bao
hilo kwa penalti, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na
Shomary Kapombe.
Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Burundi
walifanya mashambulizi mawili ya hatari zaidi, lakini sifa zimuendee ‘TZ One’,
Juma Kaseja aliyeokoa hatari hizo.
Stars
hawakucheza soka yao ya chini kutokana na hali mbaya ya Uwanja, kujaa matope,
kuwa wenye kuteleza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kutwa nzima ya leo.
Kipindi cha
pili Stars walijitahidi kutaka kusawazisha mabao hilo, lakini bahati haikuwa
yao na zaidi waliishia kukosa mabao mawili ya wazi.
Kwa matokeo
hayo, Burundi imeendelea kuongoza Kundi A, kwa pointi zao sita, mabao sita ya
kufunga na moja la kufungwa, wakati Bara inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake
tatu, Sudan ya tatu ikiwa na pointi tatu na Somalia yenye pointi moja inashika mkia.
Kikosi cha Tanzania Bara leo kilikuwa; Juma Kaseja,
Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe/Issa Rashid, Kevin Yondan, Frank
Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco, Mwinyi Kazimoto/Shaaban
Nditi na Simon Msuva/Amri Kiemba.
Burundi;
Arthur Arakaza, Gilbert Kaze, Haruna Manirakiza, Hassan Hakizimana, Emery
Nimubona, Yussuf Ndikumana, Steve Nzigamasabo, Chris Nduwarugira, Suleiman
NdikumanaChris Ndayishimiye na Amisi Tambwe.