Kim Poulsen akiongoza mazoezi ya Stars Uwanja wa Kirumba Mwanza leo |
Na Prince Akbar
MDHAMINI wa
timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars, Kilimanjaro Premium Lager amewataka wachezaji wa timu hiyo kuonyesha
nidhamu ya hali ya juu wakiwa kambini Mwanza na pia kuhakikisha wanapata
ushindi katika mechi zijazo hususani katika mechi ya Jumatano ya kirafiki dhidi
ya Harambee Stars.
Katika
taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium
Lager, George Kavishe, amesema wao kama wadhamini wana imani na timu ya taifa
na Kocha wake Kim Poulsen.
“Mechi
zilizochezwa mpaka sasa hivi tangu tumechukua udhamini zinaridhisha kwa kuwa
tumeona kiwango cha timu kikikua siku hadi siku..tuna imani mechi ya Jumatano
dhidi ya Harambee Stars tutashinda,” slisema Bwana Kavishe.
Alisema moja
ya vitu ambavyo wachezaji wanatakiwa kuzingatia sana ni nidhamu nje na ndani ya
uwanja kwani mpira ndio ajira yao kwa hivyo lazima waitetee na kuilinda vizuri.
“Kocha wa
sasa hivi anazingatia sana nidhamu na hili lina umuhimu sana katika soka hata
uwende wapi duniani..unaweza kuwa mchezaji mzuri sana lakini bila nidhamu kocha
anaweza kukuacha katika kikosi chake na kuwachezesha wachezaji wenye nidhamu,”
alisema.
Bwana
Kavishe aliendelea kusema kuwa wamefurahishwa na kitendo cha TFF kuipeleka timu
Mwanza kucheza mechi ya kirafikii dhidi ya Kenya na pia kujiandaa na mashindano
ya CECAFA Challenge yanayotarajia kuanza Jijini kampala tarehe 24 mwezi huu.
“Hali ya
hewa ya Mwanza na ya Kampala hazipishani sana kwa hivyo tunaamini huu ulikuwa
uamuzi sahihi kabisa ili wachezaji wazoee hali ya hewa, alisema.
Stars
inashuka dimbani Jumatano saa kumi alasiri dhidi ya Harambee Stars ya Kenya
katika Uwanja wa Kirumba. Tangu Stars ipate mdhamini mpya, Kilimanjaro Premium
Lager, imeshacheza dhidi ya Ivory Coast, Msumbiji, Botswana na Namibia .
Kilimanjaro
Premium Lager imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni mbili kuidhamini Taifa Stars
kwa miaka mitano ijayo.