John Bocco 'Adebayor' ataongoza safu ya ushambuliaji Stars leo? |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
TIMU ya
taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars leo inatarajiwa kuanza kampeni zake
za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker
Challenge leo itakapomenyana na Sudan kuanzia saa 12:00 jioni Uwanja wa
Mandela, Namboole mjini hapa.
Mchezo huo,
utatanguliwa na mchezo mwingine wa Kundi B kati ya Somalia na Burundi, kuanzia
saa 10:00 jioni kwenye Uwanja huo huo.
Kocha wa Kilimanjaro
Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesikitishwa na kutowasili kwa washambuliaji Mbwana
Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
“Mbwana
Samatta na Thomas Ulimwengu wanaweza wasicheze katika mechi ya kwanza kwa
sababu hawajafika, lakini mimi nikiwa kocha nimejiandaa vizuri na nina imani na
wachezaji waliopo,” alisema.
“Nina imani
TFF wanafuatilia suala hili na wachezaji hawa watajiunga na wenzao hivi
karibuni lakini hii haituzuii kufanya vizuri kwani tumejiandaa vizuri,”
alisema.
Alisema
wachezaji wote wana hali nzuri na wana ari ya kushinda mechi yao ya kwanza
dhidi ya Sudan ambazi zimo katika Kundi B pamoja na Burundi na Somalia ambazo
zitacheza leo pia.
Hata hivyo,
jana Kili Stars walilalamikia Uwanja mbovu wa Chuo Kikuu cha Kampala Kampasi ya
Biashara, waliopelekwa kufanya mazoezi kujiandaa na mechi ya leo.
Ofisa Habari
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura aliwasilisha malalamiko
hayo kwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Rodgers Mulindwa
ambaye ameahidi kuyafanyia kazi.
“Tutalifanyia
kazi suala hilo, tutakuwa na kikao kesho (leo) litawasilishwa na litapatiwa
usumbufu, mwanzo huwa na matatizo, lakini mambo yatakuwa mazuri,”alisema
Mulindwa.
Hata hivyo,
inashangaza Stars kupelekwa katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Kampala Kampasi ya
Biashara, wakati kwenye mpango wa awali kabisa wa FUFA ilitakiwa kufanya
mazoezi kwenye Uwanja wa Nakawa.