Mashabiki wanaoiunga mkono Stars mjini hapa |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
MASHABIKI wa
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars waliopo hapa, wameliomba Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kuwatumia wachezaji wa timu hiyo viatu vya kuchezea kwenye mvua,
kabla ya mechi ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati, CECAFA Tusker Challenge Jumamosi.
Wakizungumza
baada ya mechi ya jana dhidi ya Burundi, ambayo Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, walichapwa 1-0 kwenye
Uwanja wa Mandela, Namboole mjini mashabiki hao walisema hali ya hewa ya mji
huu kwa sasa itaendelea kuwa ya mvua na TFF inapaswa kuchukua tahadhari baada
ya matokeo ya jana.
“Leo
tumefungwa kwa sababu Uwanja ulikuwa unateleza kutokana na mvua na wenzetu
Burundi walikuwa wana viatu vya mvua, kwa hivyo Uwanja haukuwasumbua, sasa na
sisi lazima wachezaji wetu wapatiwe viatu hivyo,”alisema Ally Abubakar aliyetoka River Side, Ubungo, Dar es Salaam kuja
kuishangilia timu ya taifa.
Mbaya wa
Stars jana, alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam,
Suleiman Ndikumana aliyefunga bao hilo dakika ya 52, katika mchezo huo wa Kundi
B, uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole.
Burundi
walipata bao lao kwa penalti jana Nahodha huyo wa Burundi, anayechezea Inter
Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, akifunga baada ya yeye mwenyewe kuangushwa
kwenye eneo la hatari na Shomary Kapombe.
Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Burundi
walifanya mashambulizi mawili ya hatari zaidi, lakini sifa zimuendee ‘TZ One’,
Juma Kaseja aliyeokoa hatari hizo.
Stars
hawakucheza soka yao ya chini kutokana na hali mbaya ya Uwanja, kujaa matope,
kuwa wenye kuteleza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kutwa nzima ya leo.
Kipindi cha
pili Stars walijitahidi kutaka kusawazisha mabao hilo, lakini bahati haikuwa
yao na zaidi waliishia kukosa mabao mawili ya wazi.
Kwa matokeo
hayo, Burundi imeendelea kuongoza Kundi A, kwa pointi zao sita, mabao sita ya
kufunga na moja la kufungwa, wakati Bara inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake
tatu, Sudan ya tatu ikiwa na pointi moja sawa na Somalia.