Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
BARAZA la
Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limezihamisha mechi za mwisho
za Kundi B na C Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker
Challenge kutoka Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa hadi Uwanja wa Lugogo,
uliopo katikati ya mji ambao ni mfano wa viwanja kama TCC Chang’ombe au Leaders
Club pale Dar es Salaam.
Katibu wa CECAFA,
Nicholas Musonye amewaambia Waandishi wa Habari leo katika Mkutano uliofanyika
ofisi za Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), kwamba sababu ya kuzihamishia mechi
hizo huko ni hali mbaya ya Uwanja wa Namboole kwa sasa kutokana na mvua.
“Tunataka
Uwanja wa Namboole upumzike, kwa hivyo mechi zote za mwisho za Kundi B na C
zitachezwa Lugogo,”alisema Musonye, raia wa Kenya.
Aidha,
Musonye alisema kwamba mechi ya Robo Fainali itakayoihusisha Uganda, itachezwa
Jumanne kwenye Namboole, wakati mechi nyingine za hatua hiyo zitachezwa Lugogo.
Hata huvyo,
Musonye amesitikitishwa na mahudhurio ya watu kwenye mechi za mashindano ya
mwaka huu kuwa madogo na kuvitaka vyombo vya habari kuhamasisha zaidi watu
kujitokeza uwanjani.
“Nadhani
Waganda wamesononeshwa na matokeo ya timu yao kutofuzu Fainali za Mataifa ya
Afrika dakika za mwishoni, hii kwa kweli imewafanya wapoteze hamu na mpira
kidogo,”alisema.
Uganda ilifungwa
1-0 na Zambia katika mechi ya kwanza ya Raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza
fainali za mwakani za Mataifa ya Afrika na katika marudiano nayo ikashinda 1-0
nyumbani, kabla ya kutolewa kwa penalti.
Hii ilikuwa
mara ya pili mfululizo kwa Uganda kuzikosa fainali za AFCON dakika za mwishoni,
kwani hata kuelekea fainali zilizopita mwaka jana Equatorial Guinea na Gabon,
ilikomolewa na Kenya katika mechi ya mwisho nyumbani.
Kundi A,
linatarajiwa kuhitimisha mechi zake leo, kwa wenyeji na mabingwa watetezi,
Uganda, The Cranes kucheza na Sudan Kusini, saa 12:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa
na mechi kati ya Kenya, Harambee Stars na Ethiopia Uwanja wa Mandela.
Kesho, saa
8:00 mchana, Tanzania Bara itamenyana na Somalia Lugogo na baadaye saa 10:00,
Rwanda itacheza na Eritrea wakati keshokutwa, Sudan itaanza na Burundi saa 8:00
mchana na baadaye saa 10:00 jioni Malawi watamenyana na Zanzibar
Lugogo.