Kim Poulsen akijadiliana jambo na msaidizi wake, Sylvester Marsh Uwanja wa Namboole jana |
Na Boniface Wambura,
Kampala
TIMU ya soka
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajia kuingia kambini baada ya
kumalizika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge inayoendelea Uwanja wa Mandela ulioko Namboole jijini Kampala,
Uganda hadi Desemba 8 mwaka huu.
Kwa mujibu
wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen, ambaye anakiongoza kikosi cha Bara,
Kilimanjaro Stars kwenye mashindano haya, Stars itaingia kambini kujiandaa kwa
ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia, Chipolopolo
itakayochezwa Desemba 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya
pambano dhidi ya Chipolopolo, wachezaji watapata mapumziko ya wiki mbili kabla
ya kuingia tena kambini Januari 6 hadi 20 mwakani kwa ajili ya mechi nyingine
za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia
dhidi ya Morocco.
Kim
anatarajia kuongeza kipa mmoja kwenye kikosi chake ili kuwasaidia Nahodha Juma
Kaseja na Deogratias Munishi pamoja na chipukizi kadhaa kutoka timu za taifa za
vijana za Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys.
Vilevile Kim
anafuatilia wachezaji wengine kwenye timu ya Zanzibar, Zanzibar Heroes waliopo
kwenye Tusker Challenge pia katika kundi C pamoja na timu za Eritrea, Malawi na
Rwanda