Wachezaji wa Simba na Azam |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC hawajawasimamisha kipa wao Mghana, Yaw Berko na beki
Stefano Mwasyika, ila wameamua kutowatumia wakiamini wanawahujumu wakitumiwa na
Simba na Azam.
Simba wamewasimamisha Juma Nyosso na Haruna Moshi, wakiamini wanatumiwa
na Yanga na Azam kuihujumu timu yao.
Na leo, Azam wamewasimamisha Deo Munishi ‘Dida’, Said Mourad
na Erasto Nyoni wakiamini wanatumiwa na Simba na Yanga kuihujumu timu hiyo.
Hizi ni klabu tatu ambazo zinachuana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara na kwa sasa ndizo zinaibeba soka ya Tanzania.
Naheshimu mchango wa timu hizi, ambao zinatoa wachezaji wengi
timu ya taifa na hata kikosi cha sasa ukikitazama, wachezaji wote wametoka timu
hizo, kasoro wawili tu, waliotoka Mtibwa Sugar.
Sasa kama tunazitegemea timu hizi kutuzalishia wachezaji bora
na zenyewe zinatuhumiana kwa michezo michafu, je soka yetu inaelekea wapi? Kama timu yetu ya taifa, inaundwa na
wachezaji ambao hawaziwezeshi timu zao kushinda kwa uwezo bali kwa kuachiwa na
wapinzani, je soka yetu inaelekea wapi?
Nadhani, umefika wakati sasa chombo chenye mamlaka ya juu katika
soka ya Tanzania kikachukua hatua. Chombo hicho si kingine, bali Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF).
Muda mrefu wadau wanapiga kelele, juu ya rushwa katika soka
ya Tanzania na mara ya mwisho rais wa TFF, Leodegar Tenga akasema ni vigumu wao
kupambana na rushwa bila ushirikiano na idara husika kwa maana ya jeshi la Polisi.
Lakini kama Azam, Simba na Yanga zote zinachukua hatua dhidi
ya wachezaji wao kwa madai ya kununuliwa, TFF inaona ugumu gani kulifanyia kazi
suala hilo?
Kama viongozi wa klabu wanawahukumu wachezaji bila ushahidi,
TFF iwaite wote na kuwahoji kwa umakini, kuomba vielelezo na ushahidi
walioutumia kuwachukulia hatua wachezaji hao.
Kama ni ushahidi wa mazingira tu, au hisia basi viongozi
watahitaji kuelimishwa. Nimependezewa kidogo na hatua ya Yanga, hawajawasimamisha
wala kuwafukuza Berko na Mwasyika, bali wamewahamishia benchi na ikitokea wakapata
nafasi tena wanaweza kujiuliza.
Lakini Azam na Simba wamekwenda mbali zaidi- ila kitu rahisi
kwangu kuamini hapa ni kwamba, inawezekana timu zote hizi zinafanyiana mchezo
mchafu na mtu anapozidiwa kete, anachukua hatua ili kutengeneza kinga ya kesho.
Wanaweza kuchukua hatua hata bila ushahidi wa kutosha, lengo tu
ni kutengeneza mazingira ya wachezaji wengine kuogopa kesho kutumiwa. Ila sasa kwa
staili hii soka yetu inaelekea wapi? Tutafakari na tuchukue hatua.