KLABU ya Yanga, imetangaza kuwa na ziara ya nchini Uturuki
kwa wiki mbili, kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, pamoja na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame mwakani.
Na Mahmoud Bin Zubeiry |
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad
Bin Kleb alisema mapema wiki hii, kwamba ziara hiyo itakuwa kati ya Desemba
na Februari 25, mwakani.
Alisema pendekezo la kambi hiyo lilitolewa na kocha mkuu wa
Yanga, Mholanzi Ernie Brandts ambaye ana uzoefu na nchi hiyo ambayo ina vitu
vinavyostahili kwa ajili ya timu kuweka kambi.
Alisema ikiwa huko timu hiyo inatarajiwa kucheza mechi mbili
za kitrafiki na timu zitakazotajwa baadaye.
Ahadi ya ziara ya Ulaya, inakuja siku chache tu, baada ya
ahadi nyingine nzito zaidi kutolewa na uongozi wa klabu hiyo, ujenzi wa Uwanja
mpya wa kisasa wa klabu hiyo, utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki kati ya
30,000 na 40,000.
Ahadi zote hizi, zinakuja wakati klabu hiyo ikielekea katika
Mkutano wake Mkuu wa kwanza wa mwaka, tangu kuingia madarakani kwa uongozi mpya
chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Mehboob Manji Julai 14, mwaka huu.
Tayari Yanga wametangaza Mkutano Mkuu wa klabu hiyo
utafanyika Desemba 8, mwaka huu katika ukumbi wa Dar Live, Mbagala, Dar es
Salaam.
Nianze tu kwa kusema, mimi ni miongoni mwa watu ambao wana
imani kubwa na uongozi wa sasa wa Yanga chini ya Mwenyekiti Manji na ninaamini
juu ya mikakati na ahadi zao.
Lakini siku zote, watu wanapoingia katika uongozi wa soka
nchini, mara nyingi huwa wanabadilika na kufuata mkumbo wa ubabaishaji. Sina
shaka na viongozi wa Yanga juu ya hilo, lakini nataka kuendelea kuwapa
tahadhari.
Wiki iliyopita, nilizungumzia ahadi ya Manji kujenga Uwanja,
nikasema Juni mwakani ambayo Mwenyekiti huyo ameahidi ujenzi utaanza, itafika
tu kwa sababu siku hazigandi.
Manji alisaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing
Constructions Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa
ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda, unaomilikiwa na klabu hiyo.
Manji alisaini makubaliano hayo na Meneja Mkuu wa Kampuni
hiyo, David Zhang, mbele ya Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu hiyo,
makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
Katika makubaliano hayo, ilielezwa ujenzi huo wa Uwanja
utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 utaanza rasmi Juni
mwakani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini
makubaliano hayo juzi mchana, Alhaj Manji alisema kwamba wanafurahi kuanza
safari ya ujenzi wa Uwanja wao na anaamini huo ni mwanzo wa mzuri wa mipango
yao ya kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Beijing Constructions
Engineering Group alisema wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa
uwanja na klabu ya Yanga.
Alisema wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya
ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza
mechi ya kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini
ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.
Nilikumbusha kwamba, Manji si Mwenyekiti wa kwanza wa Yanga
kutoa ahadi ya kujenga Uwanja wa Kaunda na wakati juzi mkandarasi alifanya
vipimo, nataka niwakumbushe tu wasomaji wangu, wakati Tarimba Abbas, Francis
Kifukwe wakiwa viongozi wakuu wa klabu hiyo, walikwenda wakandarasi kupima
Jangwani.
Huo ni wakati ambao haijafikiriwa kama iko siku itatokea timu
inaitwa Azam FC na leo klabu hiyo ina miaka sita, lakini Uwanja wa Kaunda upo
kama alivyouacha marehemu Tarbu Mangara, tena umezidi kuchakaa kwa kukosa japo
matunzo tu.
Azam FC leo ina Uwanja wa maana na akademi, ambayo hadi
Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele alipozuru nchini aliusifia.
Nina kila sababu ya kumuamini Manji, kwa sababu kila
ukiitazama Yanga ya leo, bila ya yeye sijui ingekuwaje.
Manji aliingia Yanga mwaka 2006 baada ya jitihada
zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa
marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya Waandishi
wa Habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia
Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya
uongozi wa Francis Kifukwe.
Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame
ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”,
na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga tangu kama mfadhili hadi sasa
Mwenyekiti.
Hadi sasa, Manji ameingia kwenye historia Yanga kama miongoni
mwa watu muhimu kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo, bila hata ya ahadi ya Uwanja
na Ulaya.
Kihistoria mara nyingi, inapokaribia mikutano ya wanachama,
viongozi waliotangulia Yanga walikuwa wakitoa ahadi nzuri tamu, ili kuifanya
mikutano iwe miepesi.
Na hiyo ni desturi ambayo wanayo hata wapinzani wao wa jadi,
Simba SC haswa katika kipindi hiki, ambacho wanaongozwa na Mwenyekiti ‘mjanja
mjanja’ Alhaj Ismail Aden Rage.
Narudia kusema, bado siamini kama uongozi wa Yanga chini ya
Manji, utakuwa kama tawala zilizopita, zilizoiendesha klabu kisanii.
Nina imani na Manji na safu yake nzima ya uongozi kwamba ni
watu ambao wana mikakati waliodhamiria kuitekeleza ili kuleta mageuzi ndani ya
Yanga. Sitaki kuamini kama ahadi hizi ni danganyo toto ya mkutano Mkuu!
Wasalam.