Okwi |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
EMMANUEL
Okwi hakucheza mechi ya jana wakati timu yake ya taifa, Uganda inafuzu kwa
asilimia 100 hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati, CECAFA Tusker Challenge kutokana na maumivu ya jino.
Okwi alikaa
jukwaani kabisa katika mechi ya jana na alipoulizwa na BIN ZUBEIRY sababu ya
kutocheza mechi ya jana, alisema; “Jino linaniuma ndiyo maana leo sipo
kabisa,”alisema mshambuliaji huyo wa Simba SC ya Dar es Salaam.
Hata hivyo,
Okwi alisema anaendelea vizuri na ana matumaini katika Robo Fainali atarejea
kutetea hadhi ya Uganda.
Uganda jana
ilishinda mechi yake ya tatu mfululizo na ya mwisho ya Kundi A, mabao 4-0 dhidi
ya Sudan Kusini na kutinga Robo Fainali kwa kishindo, ikiwa haijafungwa hata
bao moja na imekusanya pointi zote tisa.
Uganda na
Kenya wamefuzu moja kwa moja, wakati Ethiopia walioshika nafasi ya tatu
watasubiri hatima yao kufuzu kama mmoja wa washindi wa watatu bora kutoka
makundi yote, A, B na C.
Mabao ya
Uganda jana yalifungwa na Brian Umony mawili katika dakika za 23 na 39, Robert
Ssentongo dakika ya 47.
Katika mechi
ya kwanza, Kenya ilishinda 3-1 dhidi ya Ethiopia, mabao ya Ramadhan Mohamed
Salim, Clifton Miheso na David Ochieng, wakati la Ethiopia lilifungwa na Gatech
Panom Yietch.
Michuano
hiyo, itaendelea leo kwa mechi za Kundi B na C, saa 8:00 mchana, Tanzania Bara
watamenyana na Somalia Uwanja wa Lugogo na baadaye saa 10:00, Rwanda itacheza
na Eritrea wakati Sudan itaanza na Burundi saa 8:00 mchana Uwanja wa
Wankulunkulu na baadaye saa 10:00 jioni Malawi watamenyana na Zanzibar
Wankulunkulu.