Wachezaji wa Simba |
Na Prince Akbar
SIMBA SC imeendelea kubaki mkoani Morogoro, baada ya sare ya
1-1 na Polisi juzi, kujiandaa na mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
humo.
Simba imeweka kambi Usambara Hotel, maeneo ya Nane Nane mkoani humo, huku
ikijifua kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Wekundu hao wa Msimbazi, wamepania kushinda mechi ya kwanza
nje ya Dar es Salaam, baada ya awali kutoa sare katika mechi zake zote za
ugenini.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba ilitoka sare za bila
kufungana na wenyeji Coastal Union na Mgambo JKT kabla ya juzi kufungana 1-1 na
Polisi, tena yenyewe ndio ikihaha hadi kipindi cha pili kukomboa bao, baada ya
Mokili Rambo kutangulia kuwafungia Maafande hao kipindi cha kwanza.
Mkombozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, alikuwa ni kiungo Amri
Kiemba juzi, ambaye hilo linakuwa bao lake la tano msimu huu.
Pamoja na hayo, Simba inajivunia kuwa timu pekee ambayo hadi
sasa haijapoteza mechi hata moja katika Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa
pointi zake 23 sawa na Yanga, baada ya kucheza mechi 11, lakini ina wastani
mzuri zaidi wa mabao.
Zaidi ya sare hizo tatu, Simba ilitoa sare nyingine mbili Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba 2-2 na Yanga SC,
wapinzani wao wa jadi, 1-1.