Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Simba imesema haiko tayari kucheza mechi yake ya
mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara siku tofauti
na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limetangaza
kuzirudisha nyuma kwa siku moja mechi zote za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi
Kuu, kutoka Jumapili wiki hii hadi Jumamosi, kasoro mechi ya Yanga na Coastal
Union pekee, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Na sababu za kutorudishwa nyuma kwa mechi ya Yanga ni kwa
kuwa Jumamosi kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo, Uwanja wa Mkwakwani, kati
ya Mgambo JKT na Azam FC.
Lakini Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN
ZUBEIRY leo kwamba hawako tayari kucheza siku tofauti na Yanga kwa
sababu ya upinzani uliopo baina yao katika mbio za ubingwa, kwani wanahofia
mchezo mchafu.
“Unajua bwana ligi hii ilipofikia ni pabaya, haiwezekani
uzichezeshe Simba na Yanga siku tofauti, hivyo sisi tunawaandikia barua TFF
kuwataarifu kwamba hatuko tayari kwa mabadiliko hayo,”alisema Kamwaga.
Kulingana na mabadiliko hayo, Simba sasa itamaliza mzunguko
wa kwanza wa Ligi Kuu Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Toto
Africans, wakati Yanga itamaliza na Coastal Mkwakwani.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi tatu za viporo
kuchezwa kwenye viwanja vitatu tofauti.
Wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Simba, Mtibwa
Sugar leo wataikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Coastal Union nao watashuka kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
kumenyana na Polisi Morogoro, huo ukiwa mchezo wa kwanza tangu wafungwe mabao
4-1 na Azam wiki iliyopita
Azam FC, wakiwa na kumbukumbu ya kutandikwa mabao 2-0 tena
wakichezewa soka ambayo hawajawahi kuiona kwa timu nyingine yoyote ya Tanzania,
wao watakuwa kwenye Uwanja wao wa Chamazi, kumenyana na JKT Oljoro
Mechi nyingine za Jumamosi ni Mgambo JKT na Azam FC Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga, African Lyon na Mtibwa Sugar Chamazi, Dar es Salaam, Prisons
na JKT Ruvu Sokoine, Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro, Kaitaba, Bukoba na
JKT Oljoro na Ruvu Shooting Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.