NILIPOFANYA naye mahojiano mwaka jana, kuna swali nilimuuliza
kiungo Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, je angependa mtoto wake pia acheze
soka?
Na Mahmoud Zubeiry |
Wakati namuuliza, jibu nililotarajia ni kwamba Haruna
angeniambia ndiyo, atapenda mwanawe aendeleze jina lake kupitia soka, lakini
ilikuwa tofauti.
Alisema asingependa mwanawe acheze soka, kwa sababu huu ni
mchezo wenye machungu mengi sana, ambayo hapendi mtoto wake akutane nayo.
Ni kitu ambacho kilikuwamo akilini mwangu, lakini sikukitilia
maanani, ila sasa nasema ni kweli, soka ni mchezo wenye machungu mengi sana.
Hilo hata Abedi Ayew Pele, mwanasoka bora wa zamani Afrika
pamoja na kuwarithisha wanawe mchezo huo, lakini anajua, soka ina machungu
mengi. Ndiyo, wakati fulani.
Ila soka pia ina tamu nyingi pia. Kushinda mataji, kulipwa
fedha nyingi, kuwafanya mamilioni washerehekee wakitaja jina lako, kuwa maarufu
na tajiri.
Lakini hayo, si sana kwa huku kwetu Afrika, hususan Tanzania.
Soka ina machungu mengi sana na inataka moyo kumruhusu mwanao kucheza soka,
ikiwa wewe ulicheza na umekutana na hayo machungu.
Na hapo siwezi kujiuliza sana kwa nini simuoni uwanjani mtoto
wa Golden Boy wetu wa miaka ya 1980, Zamoyoni Mogella ama mtoto wa Khalid Abeid
au mtoto wa Leodegar Tenga.
Na hapo hapo, naona ipo kila sababu ya kuwapongeza watu kama
Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Mao Mkami ‘Ball Dancer’ ambao leo vijana wao
wanaendeleza majina yao uwanjani. Walikuwa wana moyo sana kuwaruhusu watoto wao
kucheza, ikiwa wao walipambana na machungu ya soka ya Tanzania.
Soka ya Tanzania imejaa majungu, fitina, dhuluma, wizi na
uzandiki na katika haya yote, muathirika wa kwanza ni mchezaji.
Kabla ya kumlaumu mchezaji wa leo wa Tanzania kwa nini
hachezi Ulaya kama wenzake wa nchi nyingine za Afrika, natazama mazingira
yaliyomuibua na yanayomlea, sioni dalili za kumfikisha huko.
Mchezaji anaibuka katika mazingira ya tabu sana, kucheza soka
katika mazingira hatarishi, kutopewa sapoti za muhimu kama vifaa vya mazoezi,
lishe bora na kadhalika.
Na anapokuwa katika mazingira hayo hayo, hata akipata nafasi
ya kusema ajaribu kutimiza ndoto zake, anakutana na changamoto nyingine za
kumuumiza zaidi.
Nimeanzia mbali sana leo na ninadhani ninawapa tabu kidogo
wasomaji wangu kuelewa naelekea wapi, ila naamini tunaelewana.
Mungu amrehemu, Athumani Mambosasa, huyu alikuwa kipa hodari
wa Simba SC miaka ya 1970 na moja ya sifa zake kubwa ni kudaka hadi kuiwezesha
klabu hiyo kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974.
Leo hii hata ukikutana na mashabiki wa Simba wale wa enzi
hizo, si hawa wa leo oye oye, watakupa sifa za Mambo na ujasiri wake.
Watakuambia sijui alitishiwa bastola aachie mabao Misri, lakini akagoma.
Pamoja na sifa hizo, Mambo ameaga dunia hana furaha na Simba.
Kwa nini? Alifukuzwa akiambiwa amehujumu timu. Mambo anakwenda kwenye Fainali
za Mataifa ya Afrika mwaka 1980, alikuwa hana timu.
Alikuwa amekwishaacha soka yupo zake Arusha amepumzika. Baada
ya kufukuzwa Simba mwaka 1975, akidaiwa kuhujumu timu dhidi ya Yanga kipigo cha
mabao 2-0 Zanzibar fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, siku hizi
tunaita Kombe la Kagame, Mambo aliungana na wachezaji waliojitoa Yanga kufuatia
mgogoro wa mwaka 1976 kwenda kuasisi timu ya Nyota ya Morogoro.
Lakini wachezaji wa Yanga walipokuja Dar es Salaam kuasisi
Pan Africans mwaka 1978, yeye akaamua kuacha soka.
Taifa Stars ilipokuwa kambini Arusha kujiandaa na Fainali za
Nigeria mwaka 1980, ndipo kocha akamkuta huko na kumuita mazoezini, akaridhika
naye akaenda naye kwenye faianli hizo na aliporejea huko, akastaafu moja kwa
moja.
Mwameja Mohamed, pamoja na makubwa aliyoifanyia Simba kuipa
mataji kibao na kuifikisha fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, lakini hadi leo
nina barua yake ya kujiondoa Simba mwaka 1999 baada ya kusononeshwa na shutuma
za kudaiwa kuhujumu timu.
Lakini bado soka ina machungu mengi zaidi ya haya kuambiwa
umehujumu timu. Muda mrefu mchezaji anakuwa mbali na familia yake, analazimika
kujihimu kila siku kwa ajili ya mazoezi, mwili unachoka wakati mwingine, lakini
anajituma.
Zamani, kama mechi kesho, mchezaji hata akifiwa na baba au
mama yake mzazi, kama timu inamtegemea haambiwi hadi baada ya mechi, ili
aitumikie timu kwanza.
Wale maelfu wanaokwenda uwanjani ni kwa sababu ya wachezaji-
sasa nenda kwenye suala la maslahi yao, hayo ni machungu mengine ya soka ya
Tanzania.
Toto Africans wanacheza Ligi Kuu, lakini wana miezi minne
hawajalipwa mishahara, wakati wachezaji wake wengi ni vijana wadogo na wengine
ni wanafunzi, wanatoka kwenye familia duni wanategemea fedha hizo hizo ziwasomeshe.
Na hapo utastaajabu nini mwanasoka wa kimataifa wa zamani
Tanzania anaomba nauli ya daladala?
Sekilojo Chambua alipata nafasi ya kwenda kucheza soka ya
kulipwa Uarabuni mwaka 1998 akakataa ili aendelee kucheza Yanga, ila
alipostaafu muulize alifanyiwa nini? Unaweza kumtoa machozi.
Kweli soka ina machungu mengi. Juma Kaseja amekuwa kipa wa
kwanza Simba SC tangu mwaka 2003, akimpokea Mwameja Mohamed na amekuwa na
mchango mkubwa sana kwenye timu hiyo.
Leo ameomba kujitoa kwenye timu, baada ya kufanyiwa fujo na
mashabiki, kufuatia Simba kufungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar yeye akiwa
langoni.
Hata kama kweli kuna bao la kizembe alifungwa, Juma ni
binadamu na mchezo wenyewe huu si bao. Kashfa nyingine anazopewa huwezi kuona
zinatoka wapi, Juma hajipangi mwenyewe kwenye kikosi cha kwanza. Walimu
wanampanga.
Na si walimu wa Simba tu, bali hata walimu wa timu ya taifa,
kwao huyo ndiye kipa bora. Leo Juma hana raha na Simba na bila shaka atakuwa
analia zaidi akikumbuka jinsi alivyoipigania kupata mataji kibao.
Leo sasa nimemuelewa Niyonzima, soka ina machungu mengi. Pole
Kaseja.