Kim Poulsen jana |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA Mkuu
wa timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, raia wa Denmark,
amesema kwamba bado ana matumaini ya kutinga Robo Fainali ya michuano ya Kombe
la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge licha ya jana
kuchapwa 1-0 na Burundi.
Mbaya wa Kim
na Stars jana, alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam,
Suleiman Ndikumana aliyefunga bao hilo dakika ya 52, katika mchezo huo wa Kundi
B, uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY baada ya mechi ya jana, Poulsen alisema kwamba anaamini
wakishinda mechi ya mwisho dhidi ya Somalia, watasonga mbele.
Hata hivyo,
Kim alisema haidharau Somalia kwani imeonyesha mchezo mzuri katika mechi zake
zote mbili pamoja na kufungwa.
“Nina muda
mzuri kidogo wa kujiandaa na mchezo huo hadi Jumamosi, tutajiandaa vizuri na
nina matumaini ya kushinda,”alisema.
Akizungumzia
mchezo wa jana, Kim alisema walitengeneza nafasi nyingi nzuri, lakini wakashindwa
kuzitumia, mipira ikigonga mwamba na mingine ikiokolewa ikiwa inaelekea
nyavuni, hivyo hana wa kumlaumu kwa matokeo hayo, bali habati haikuwa yao jana.
Burundi
walipata bao lao kwa penalti jana Nahodha huyo wa Burundi, anayechezea Inter
Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, akifunga baada ya yeye mwenyewe kuangushwa
kwenye eneo la hatari na Shomary Kapombe.
Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Burundi
walifanya mashambulizi mawili ya hatari zaidi, lakini sifa zimuendee ‘TZ One’,
Juma Kaseja aliyeokoa hatari hizo.
Stars
hawakucheza soka yao ya chini kutokana na hali mbaya ya Uwanja, kujaa matope,
kuwa wenye kuteleza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kutwa nzima ya leo.
Kipindi cha
pili Stars walijitahidi kutaka kusawazisha mabao hilo, lakini bahati haikuwa
yao na zaidi waliishia kukosa mabao mawili ya wazi.
Kwa matokeo
hayo, Burundi imeendelea kuongoza Kundi A, kwa pointi zao sita, mabao sita ya
kufunga na moja la kufungwa, wakati Bara inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake
tatu, Sudan ya tatu ikiwa na pointi moja sawa na Somalia.
Kikosi cha Stars
jana kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe/Issa
Rashid, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco,
Mwinyi Kazimoto/Shaaban Nditi na Simon Msuva/Amri Kiemba.