Kocha Kili Stars, Kim Poulsen |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen
amesema kwamba bado anawahitaji mno washambuliaji Mbwana Ally Samatta na Thomas
Emanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na iwapo
hawatajiunga kabisa na kikosi chake, watamuweka katika wakati mgumu.
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY jana mjini hapa, baada ya mchezo dhidi ya Sudan wa Kundi B Kombe
la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, ambao
walishinda 2-0, Kim alisema jitihada za kuwaomba Mazembe wawaruhusu wachezaji
hao zinaendelea.
“Sijui
itakuwaje wasipokuja, itanibidi tu niwatumie wachezaji hawa hawa waliopo, najua
nina mshambuliaji mmoja, lakini nitawatumia hawa hawa waliopo, Simon Msuva
anaweza akawa mshambuliaji, nitafanyeje,”.
“Siwezi kuita
mchezaji mwingine kutoka nyumbani kwa sasa, kwa sababu mtu lazima umuone uwezo
wake, huwezi kumuita tu, kwa hivyo naomba Mungu tu Samatta na Ulimwengu waje,”alisema
Kim.
Stars inayodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager, jana ilianza vema kampeni zake za kuwania Kombe
la Challenge, baada ya kuichapa mabao 2-0 Sudan kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole,
Kampala, Uganda.
Ushindi huo,
unaiweka Stars katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, nyuma ya
Burundi inayoongoza kwa wastani wa mabao.
Hadi
mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yote yakipachikwa kimiani na
mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyetumia vema krosi za
Mrisho Khalfan Ngassa.
Bocco
alifunga bao la kwanza Bocco aliiwahi vema krosi ya Ngassa aliyewatoka mabeki
wa Sudan wingi ya kushoto na kuitumbukiza kimiani dakika ya 14.
Adebayor wa
Chamazi aliwainua tena vitini mashabiki wa Tanzania dakika ya 28, akiunganisha
krosi ya Ngassa tena kutoka kule kule kushoto.
Kwa ujumla
Tanzania Bara walicheza vizuri kipindi cha kwanza, wakishambulia zaidi kupitia
pembeni, kulia Simon Msuva ambaye hakuwa na madhara sana na kushoto Ngassa
ambaye alikuwa mwiba mchungu haswa kwa Wasudan.
Pamoja na
Bara kutawala kipindi cha kwanza, lakini Wasudan walifanya mashambulizi kadhaa
ya kushitukiza na sifa zimuendee mlinda mlango Juma Kaseja, ambaye alioko
amichomo miwili ya hatari mno.
Kipindi cha
pili Stars, inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen iliendelea kutawala mchezo,
lakini safu ya ulinzi ya Sudan iligangamala.
Kikosi cha
Stars jana kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kevin
Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar/Amri Kiemba, John Bocco, Mwinyi Kazimoto
na Simon Msuva/Shaaban Nditi.
Sudan; Ebd
Elrahman Ali, Moawia El Amin, Sami Abdallah, Faris Abdallah, Hamoda Bashir/Farid
Mohamed, Mohamed El Mortada, Sadam Abutalib, Mohamed Mussa Idris, Modathir
Mohamed, Adam Sayer/Osama El Rashid na Mohamed Osman/Saed Siddig.
Katika
mchezo wa awali, Burundi walishinda mabao 5-1, mabao yake yakifungwa na Chris
Nduwarugira dakika ya 35 na 88, Yussuf Ndikumana dakika ya 41 na Suleiman
Ndikumana dakika ya 84 na 90, wakati la Somalia lilifungwa na Mohamed Jabril
kwa penalti dakika ya 55.
Matokeo hayo
yanalifanya Kundi B lizidi kuwa gumu, kwani Burundi inaongoza kwa pointi zake
tatu na mabao mengi, Tanzania ya pili kwa pointi tatu na mabao mawili- lakini
bado Sudan wanaweza kupata matokeo mazuri katika mechi zijazo.
MSIMAMO
KUNDI B:
P W D L GF GA GD Pts
Burundi 1 1 0 0 5 1 4 3
Tanzania 1 1 0 0 2 0 2 3
Sudan 1 0 0 1 0 2 -2 0
Somalia 1 0 0 1 1 5 -4 0