Kilimanjaro Stars |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen
amesema kwamba uwezo wa timu yake unazidi kukua siku hadi siku na sasa ana
matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA, Tusker Challenge.
“Tuliwafunga
Kenya, tumewafunga Sudan, timu zote nzuri, Sudan wapo juu yetu kiuwezo katika
viwango vya FIFA. Kwangu siangalii sana viwango vya FIFA, mpira ni pale
unapokuwa uwanjani,”alisema Poulsen.
Akilizungumzia
kundi lake, B lenye timu za Sudan, Somalia na Burundi, alisema ni gumu na
wanatakiwa kupambana ili kufika mbali.
Lakini
Poulsen amesema bado anawahitaji mno washambuliaji Mbwana Ally Samatta na
Thomas Emanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) , ambao wamezuiwa na klabu yao.
Kim alisema
jitihada za kuwaomba Mazembe wawaruhusu wachezaji hao zinaendelea.
“Sijui
itakuwaje wasipokuja, itanibidi tu niwatumie wachezaji hawa hawa waliopo, najua
nina mshambuliaji mmoja, lakini nitawatumia hawa hawa waliopo, Simon Msuva
anaweza akawa mshambuliaji, nitafanyeje,”.
“Siwezi
kuita mchezaji mwingine kutoka nyumbani kwa sasa, kwa sababu mtu lazima umuone
uwezo wake, huwezi kumuita tu, kwa hivyo naomba Mungu tu Samatta na Ulimwengu
waje,”alisema Kim.
Stars inayodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager, jana ilianza vema kampeni zake za kuwania Kombe
la Challenge, baada ya kuichapa mabao 2-0 Sudan juzi kwenye Uwanja wa Mandela,
Namboole, Kampala, Uganda.
Ushindi huo,
unaiweka Stars katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, nyuma ya
Burundi inayoongoza kwa wastani wa mabao.