Barthez |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA wa makipa wa Yanga, Mfaume Athumani Samatta
ameshangazwa na kitendo cha kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars,
Mdenmark Kim Poulsen kuwaita kwenye kikosi cha Bara makipa Juma Kaseja wa Simba
na Deo Munishi ‘Dida’ ambao wote hawako vizuri kwa sasa, huku akimuacha Ally
Mustafa ‘Barthez’ ambaye yuko vizuri.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Samatta alisema
Dida alidaka mechi mbili tu mwanzoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, lakini baada ya hapo amekuwa akisugua benchi na Mwadini Ally
ndiye amekuwa akidaka mechi zote za Azam.
Kuhusu Kaseja, Mfaume alisema kipa huyo kwa sasa hayuko
vizuri na amekuwa akiruhusu mabao rahisi sana, tofauti na Barthez ambaye yuko
vema mno.
“Barthez huku anapokezana na Yaw Berko kudaka, lakini amedaka
mechi zetu tatu mfululizo zilizopita na hajaruhusu bao hata moja, amedaka na
Polisi tumeshinda 3-0, amedaka na JKT Oljoro tumeshinda 1-0 na amedaka na Azam
tumeshinda 2-0 na anafanya kazi ambayo wananchi wanaiona na wanakubali,”.
“Kwa kweli mimi maoni yangu katika nafasi ya kipa, kocha
kachemka sana, tena sana. Ameita hao watu kwa sababu ya mazoea tu, hajazingatia
viwango vyao vya sasa, kwangu mimi ilipofikia Barthez ndiye Tanzania One na
hakuna ubishi,”alisema Mfaume.
Mfaume Athumani |
Jana Paulsen amemuorodhesha Kaseja katika kikosi cha wachezaji
22 watakaounda kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars kitakachomenyana na Kenya,
Harambee Stars katika mchezo wa kirafiki ulio katika kalenda ya FIFA
(Shirikisho la Soka la Kimataifa) Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wiki ijayo.
Mbali na Kaseja wa Simba, Kim aliyepandishwa kutoka timu ya
vijana mwaka huu akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Borge Poulsen
amemuita pia kipa Deogratius Mushi wa Azam FC.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Mwanza jana, Paulsen
aliwataja wachezaji wengine ni mabeki Kevin Yondan wa Yanga, Aggrey Morris,
Erasto Nyoni wa Azam FC, Issa Rashid, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe
na Amir Maftah wa Simba, wakati viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC,
Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa wa
Simba, Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo wa Yanga na Shaaban Nditi wa Mtibwa
Sugar.
Washambuliaji walioitwa na Paulsen ni John Bocco ‘Adebayor’ wa
Azam FC, Simon Msuva wa Yanga, Christopher Edward wa Simba, Mbwana Samatta na
Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
Hata hivyo, Poulsen hakuchukua wachezaji wengi wa Zanzibar kwa
sababu nao watakwenda kujiunga na timu ya Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya
Kombe la CECAFA Tusker Challenge mwishoni mwa mwezi huu mjini Kampala, Uganda. Alisema
hicho ndio kikosi anachotarajia kukutumia katika Challenge. Kambi ya timu hiyo
itakuwa mjini Mwanza, kwa kuwa ni jirani na Uganda.
KIKOSI KILI STARS;
Makipa; Juma Kaseja
(Simba SC) na Deogratius Mushi ‘Dida’
Mabeki; Kevin Yondan (Yanga), Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam
FC), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe na
Amir Maftah (Simba).
Viungo; Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC), Amri Kiemba,
Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa (Simba), Athuman
Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo (Yanga) na Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji; John Bocco ‘Adebayor’ (Azam FC), Simon Msuva (Yanga),
Christopher Edward (Simba), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa (TPM, DRC).