Okwi |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
EMMANUEL
Okwi, mshambuliaji wa Uganda, The Cranes amesema jana kocha wao Bobby
Williamson, raia wa Scotland aliwalekeza kucheza bila kutumia nguvu nyingi, ili
kutunza nguvu kwa ajili ya mechi zijazo na ndiyo maana walipata ushindi
mwembamba wa 1-0 dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mataifa
ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker, Challenge.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY baada ya mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mandela, Namboole,
Okwi anayechezea Simba SC ya Tanzania, alisema kwamba kocha wao alitaka
washinde bila kutumia nguvu nyingi, kwa kuwa mashindano bado yapo katika hatua
za awali.
“Ni kweli
bado mapema sana, mtu ukitumia nguvu nyingi unaweza kuumia na kuiachia timu
pengo, sasa kocha amekuwa makini sana na sisi tunafuata maelekezo yake. Na
amekuwa mwoga baada ya Abbel Dhaira (kipa) kuumia kwenye mechi na
Kenya,”alisema Okwi na kuongeza.
“Na
ukiangalia ni kweli, haina maana kuingia Robo Fainali wakati wachezaji wako
wengi majeruhi, hautafika mbali, na sisi lengo letu ni kutetea Kombe hapa, tena
mashindano yanafanyika nyumbani,”alisema Okwi.
Uganda jana ilishinda
1-0 na sasa inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake sita, mabao mawili ya kufunga,
haijafungwa bao hata moja, ikifuatiwa na Kenya yenye pointi tatu, mabao mawili
ya kufunga na moja la kufungwa, Ethiopia pointi tatu pia bao moja la kufunga na
moja la kufungwa na Sudan Kusini ambao hawana pointi wanashika mkia. Matokeo
hayo yanamaanisha Uganda tayari imefuzu Robo Fainali, wakati Kenya na Ethiopia
japo zina nafasi kubwa, lakini kwa uhakika zaidi ni hadi matokeo ya mechi za
mwisho za kundi hilo.