Athumani Nyamlani |
Na Princess Asia
MAKAMU wa
Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani
ameteuliwa kuwemo kwenye Ujumbe rasmi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF)
utakaosimamia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika
Januari mwakani nchini Afrika Kusini.
Ofisa Habari
wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, uteuzi huo
umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji. Ujumbe huo
wa CAF kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari
10 mwaka huu una jumla ya watu 148.
Wambura amesema
Nyamlani atakuwa miongoni mwa wajumbe watatu, watakaoshughulikia masuala ya
rufaa kwenye mashindano hayo. Wajumbe wengine ni Prosper Abega kutoka Cameroon
na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon. Nyamlani ni mjumbe wa Bodi ya Rufani ya
CAF yenye watu 12.