Haruna Niyonzima anakwenda El Merreikh |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya
Yanga imepokea ofa kutoka klabu mbili tofauti, moja ya Asia na moja ya hapa
hapa Afrika zikiwahitaji wachezaji wao mahiri wa kigeni, kiungo Haruna Niyonzima
kutoka Rwanda na mshambuliaji Didier Kavumbangu kutoka Burundi.
Habari za
ndani kutoka Yanga, zimesema kwamba, Niyonzima anatakiwa na klabu ya El
Merreikh ya Sudan, wakati Kavumbangu anatakiwa na klabu moja ya Qatar.
Tayari barua
rasmi za kuwahitaji wachezaji hao zimekwishawasilishwa Yanga na hivi sasa klabu
inaingia kwenye majadiliano ya bei na klabu hizo.
Klabu ya
Qatar, ilitangaza ofa ya dola za Kimarekani 100,000 (zaidi ya Sh. Milioni 150),
lakini Yanga imekataa dau hilo na inataka dola 300,000 (zaidi ya Sh. Milioni
450) kwa ajili ya Kavumbangu.
Kuhusu Niyonzima,
Merreikh imeomba itajiwe bei ya mchezaji huyo na Yanga. “Merreikh wana fedha,
hatuna wasiwasi nao, sisi tutaanzia dola 300,000 na hata tukishuka, si chini ya
200,000, hawa wachezaji ni lulu”kilisema chanzo kutoka Yanga.
Didier Kavumbangu anakwenda Qatar |
Haruna alisajiliwa
msimu uliopita Yanga kutoka APR ya Rwanda, wakati Kavumbangu amesajiliwa msimu
huu kutoka Atletico Olympic ya Burundi.
Kavumbangu kwa
sasa ndiye anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akiwa
ametikisa nyavu mara nane, sawa na Kipre Tcheche wa Azam FC.
Wataalamu wa
usajili wa Yanga, Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Ahmad ‘Bin Kleb’ tayari
wanajiandaa kwenda Kampala, Uganda itakapofanyika michuano ya Kombe la
Challenge kutafuta wachezaji wa kuziba nafasi za Kavumbangu na Niyonzima.
Lakini habari
zaidi zinasema nafasi ya Niyonzima itazibwa na Kabange Twite kutoka APR ya
Rwanda, ndugu wa mchezaji mwingine wa Yanga, Mbuyu Twite.