Haruna Niyonzima |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KIUNGO wa
Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amesema kwamba iwapo Yanga watakubali
ofa ya klabu ya El Merreikh ya Sudan, atakuwa radhi kuondoka klabu hiyo na
kwenda kuanza maisha mapya Khartoum.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana mjini hapa, Nahodha huyo wa Rwanda katika michuano ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge alisema
kwamba anaipenda sana Yanga lakini soka kwa sababu ni kazi yake, anaangalia
maslahi pia.
“Mimi
walinifuata Merreikh, nikawaambia nina mkataba na Yanga, wawasiliane na Yanga.
Kama Yanga watakubali, mimi nitaangalia maslahi tu, Merreikh wakinipa maslahi
mazuri kuliko nayopata Yanga sitakuwa na tatizo,”.
“Lakini
kwanza, Yanga wao wenyewe wakubali kuniuza, wakikubali mimi sina tatizo,
nawaheshimu sana Yanga wamenilea vizuri kwa kipindi chote nilichokuwa nao na
ndiyo maana uwezo wangu haujayumba,”alisema Niyonzima.
Lakini
Haruna alisema ana ofa pia ya kwenda kucheza Ubelgiji, ingawa alisema hiyo ipo
nusu kwa nusu tofauti na ya Merreikh ambao wameonyesha nia ya moja kwa moja ya
kumuhitaji.
“Kucheza
Ulaya ni kitu ambacho kila mchezaji wa Afrika anakitaka, kama Mungu atapenda
niondokee Yanga kwenda Ulaya, nitafurahi, na kama kuondokea Sudan, yote sawa,
au nitamalizia soka yangu Afrika, yote sawa pia,”alisema.
Niyonzima ni
kati ya wachezaji wa Yanga wanaong’ara katika CECAFA Tusker Challenge, wengine
wakiwa ni Hamisi Kiiza wa Uganda, Frank Domayo wa Tanzania Bara na Nadir Haroub
‘Cannavaro’ wa Zanzibar.
Niyonzima
aliyesajiliwa Yanga mwaka jana kutoka APR ya nyumbani kwao, Rwanda jana
aliiongoza nchi yake, kuifunga mabao 2-0 Malawi katika mchezo wa Kundi C,
akiifungia Amavubi bao la pili kipindi cha pili, baada ya Jean Baptiste
Mugiraneza kufunga la kwanza kipindi cha kwanza.