Mubarak Suleiman |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
Sudan, Mubarak Suleiman amesema kwamba hawakuja na kikosi chao
kamambe katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge kutokana na wachezaji wao chaguo la awali kuwa na klabu zao,
El Merreikh, Al Ahly Shandy na El Hilal kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho
la Soka Afrika.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa,
Suleiman alisema kwamba wachezaji aliokuja nao wanatoka klabu nyingine ndogo za
nchini mwao na ndiyo maana timu yao haina makali yake yaliyozoeleka.
“Tumekuja kushiriki ili kuwapa uzoefu wachezaji wengine,
hatukuja na timu yetu ya kwanza kwa sababu wachezaji wote wapo na timu zao
kwenye Kombe la Shirikisho,”alisema kocha huyo.
Hata hivyo, Suleiman alisema kwamba wamekuja hapa kushindana
na watajitahidi kadiri ya uwezo wao kupata matokeo mazuri.
“Wachezaji hawa wageni wa mashindano makubwa, lakini taratibu
watapata uzoefu na ninaamini katika mechi zijazo watafanya vizuri na tunaweza
kufika mbali,”alisema.
Sudan katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B ilifungwa mabao
2-0 na Tanzania Bara wakati mchezo wa pili, ilishinda kwa mbinde 1-0 dhidi ya
Somalia na kesho itakamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na
Burundi.
Hadi sasa uwezekano wa Sudan kutinga Robo Fainali, zaidi ni
kama mmoja wa washindi wa tatu bora- kwani kesho itamenyana na Burundi, ambayo
hadi sasa unaweza kusema ndio timu iliyoonyesha mchezo mzuri zaidi kwenye
mashindano haya, ikiwa inaongoza Kundi B.