Ngassa alivyokuwa akiteleza kushoto mwa uwanja wa namboole jana, balaa |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
SALUTI kwa
Mrisho Khalfan Ngassa. Waganda, wamekoma naye. Mashabiki wa soka Uganda,
wamekoshwa na soka ya Mrisho Khalfan Ngassa wa Tanzania Bara katika michuano ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge inayoendelea
mjini hapa.
Wakizugumza baada
ya mechi kati ya Sudan na Tanzania, mashabiki walikuwa wakimsifia mno mchezaji huyo
wa Tanzania Bara aliyekuwa amevalia jezi namba nane na kusema hawajui siku
Stars ikikutana na Uganda itakuwaje mbele ya mshambuliaji huyo wa Simba SC ya
Dar es Salaam.
Hata Waandishi
wa Habari wa Uganda, wamemsifia mno Ngassa wakisema huyo ndiye mchezaji
aliyeonyesha kiwango kikubwa zaidi cha uchezaji hadi sasa kwenye michuano hii.
Ngassa jana
alikuwa mwiba kweli mbele ya Sudan, akitengeneza mabao yote mawili ya ushindi
yaliyofungwa na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC.
Jana Ngassa
alipangwa wingi ya kushoto ambako alikuwa akiteleza kwa kasi na kutoa krosi
nzuri ambazo bahati mbaya au nzuri ni mbili tu zilizotumiwa vyema na Bocco.
Mashabiki wamemsifia
pia Ngassa kwamba si mchezaji mchoyo ambaye muda wote anafikiria zaidi kuwatengenezea
wenzake nafasi kuliko kutaka kufunga mwenyewe.
Ngassa ni
kati ya wachezaji 10 wa Simba wanaocheza michuano ya mwaka huu mjini hapa,
wengine wakiwa ni Nassor Masoud 'Cholo' (Zanzibar), Juma Kaseja
(Bara), Shomari Kapombe (Bara) Amir Maftah (Bara), Amri Kiemba, (Bara) Mwinyi
Kazimoto (Bara), Ramadhani Singano ‘Messi’ (Bara), Christopher Edward (Bara) na
Emanuel Okwi (Uganda).
Timu nyingine za Bara zenye wachezaji hapa ni Azam tisa, Mwadini Ali (Zanzibar), Abdulaghan
Gulam (Zanzibar ), Samir Haji Nuhu(Zanzibar), Aggrey Morris(Zanzibar), Khamis
Mcha 'Vialli'(Zanzibar), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Bara), Erasto Nyoni (Bara),
Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Bara) na John Bocco ‘Adebayor’ (Bara).
Yanga ina wachezaji saba, ambao ni Nadir Haroub Ali 'Canavaro'(Zanzibar),
Haruna Niyonzima (Rwanda), Hamisi Kiiza (Uganda), Kevin
Yondan (Bara), Athuman Iddi ‘Chuji’ (Bara), Frank Domayo (Bara) na Simon Msuva (Bara),
wakati Mtibwa Sugar inao
watatu Twaha Mohammed (Zanzibar), Issa Rashid (Bara) na Shaaban Nditi
(Bara), JKT Oljoro ina
mmoja Amir Hamad (Zanzibar) sawa na Coastal Union Suleiman Kassim 'Selembe' wa Zanzibar pia.