Hamisi Leon, Nahodha wa Sudan Kusini |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Sudan ya Kusini, Hamisi Leon amewataka viongozi wa Yanga waje
Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge kushuhudia uwezo wake kwa mara nyingine.
Mshambuliaji
huyo wa Waw Salam ya Sudan Kusini, alikaribia kusajiliwa na Yanga Julai mwaka
huu wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, lakini akazidiwa kete na Didier Kavumbangu aliyekuwa anachezea Atletico
ya Burundi.
Hata hivyo,
wakati huu ambao Kavumbangu yuko mbioni kuhamia Qatar anakotakiwa kwa dau zuri,
Yanga ina nafasi ya kumsajili Leon.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY katika mahojiano maalum jana, Leon ambaye ni Nahodha wa Sudan
Kusini alisema kwamba alifanya mazungumzo na Yanga alipokuwa Dar es Salaam na
amekuwa na mawasiliano nao hata akiwa Sudan.
Leon alisema
kwamba anaipenda Yanga na atafurahi siku moja akijiunga nayo, kwani anaamini
atacheza vizuri na kupata mafanikio makubwa.
“Mimi
ninajiamini nina uwezo na sibahatishi, nawaambia viongozi wa Yanga waje kuniona
tena hapa Uganda, sijui kama watavutiwa na mshambuliaji mwingine zaidi
yangu,”alisema Leon.
Leon pamoja
na kung’ara katika mchezo wa jana wa Kundi A, dhidi ya Ethiopia, lakini
alishindwa kuiepusha timu yake na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wawakilishi hao
wa CECAFA kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini.