Pele kushoto na BIN ZUBEIRY |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI
wa zamani wa kimataifa Ghana, Abedi Ayew Pele anaamini ipo siku Muafarika
atatwaa tena tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia na anaamini wakali kama yeye enzi
zake wataibuka tena kutoka barani.
Mwanasoka
huyo bora wa zamani Afrika, ambaye pia ni Balozi wa Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA), alisema hayo alipokuwa akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini
Dar es Salaam.
“Ndiyo,
Mwafrika atatwaa tena tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, na kutokana na mipango
hii mizuri ya kuwa akademi nzuri za kuzalisha vijana,”alisema Pele.
Amesema
lazima wachezaji wa sasa wa Afrika wawe na malengo baada ya kujengewa misingi
mizuri ndipo ndoto hizo zitimie.
“Kizazi
chetu, mimi na akina Rogger Milla na George Weah kilifanya vizuri sana. Kikaja
kizazi cha akina Samuel Eto’o nacho kimefanya vizuri ingawa hawakufikia rekodi
ya kizazi chetu.
Sasa
tutarajie vizazi vijavyo, vitatoa tena Mwanasoka Bora wa Dunia. Naamini hivyo
kutokana na mipango mizuri iliyopo. Lakini lazima tubadilike na tufanye kazi,
maana sisi Waafrika ni hodari sana wa kuzungumza, lakibi vitendo hakuna, lazima
tutende sasa,”alisema Pele.
Hadi sasa,
ni George Weah pekee katika wanasoka wa Afrika, aliyefanikiwa kutwaa Tuzo ya
Mwanasoka Bora wa Dunia, mwaka 1995, akimpiku Paolo Maldini wa Italia aliyekuwa
wa pili, huku Jurgen Klinsmann wa Ujerumani akiwa wa tatu. Mwaka huo huo, alisihinda
pia tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika na Ulaya.
Pele pia
alisema katika mechi ya juzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga
na Azam alivutiwa na soka, ushindani, kiwango na uwezo wa wachezaji, ingawa alimtaja
Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kuwa ndiye aliyemvutia zaidi.
Pele alisema
wachezaji wengi waliocheza juzi wana viwango vya kucheza Ulaya, ingawa
amemsifia zaidi Niyonzima, kwamba anastahili kabisa kucheza moja ya klabu kubwa
hata Ulaya.
“Aliyevaa
jezi namba nane wa Yanga, anajua sana. Niliambiwa ni Mnyarwanda, Yule kijana
mzuri sana, ni mtaalamu,”alisema Pele akizungumza na Waandishi wa Habari mchana
wa jana katika ziara yake makao makuu ya klabu ya Azam, Azam Complex, Chamazi,
Dar es Salaam.
Pele ambaye
akiwa Chamazi amejionea mambo mbalimbali, ikiwemo mradi wa maendeleo ya soka ya
vijana, Academy aliousifia sana na kusema utaleta matunda makubwa Tanzania
baadaye, alikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi Yanga ikiilaza Azam 2-0.
Akiizungumzia
Azam kwa ujumla, amesema miaka kadhaa ijayo itakuwa klabu kubwa yenye hadhi
sawa na Manchester United ya England kutokana na uwekezaji wake mzuri.
Alisema
akademi ya Azam ni nzuri na bora kuliko hata akademi yake. “Kwetu tuna akademi
nyingi, lakini nyingi ni za wawekezaji wa nje (klabu za Ulaya), lakini hii ni
ya Azam, safi sana. Akademi yangu ni ndogo tu, haiifikii hii kwa ubora, nami
nina ndoto za kufanya kitu kama hiki, nadhani nitajifunza mengi kutoka kwa
Azam,”alisema Pele.
Pele pia aliishauri
Azam kuachana na desturi ya kuchukua wachezaji wa nje ya nchi, kwani kama
wataitumia vizuri akademi yao kwa kusaka vipaji zaidi nchi mzima, mbele ya watu
zaidi ya Milioni 40 watapata wachezaji bora.
“Kama kwa
lengo la kubadilishana tu uzoefu sawa, lakini kama una kademi nzuri kama hii,
kwa nini uchukue mchezaji kutoka Ghana, hii nchi yenu ina watu zaidi ya Milioni
40, mnaweza kutengeneza wachezaji wengi wazuri na nyinyi mkauza Ulaya,”alisema
Pele ambaye ameahidi kuanzisha ushirikiano wa akademi yake na ya Azam, baada ya
kuombwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Akiizungumzia
Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuona mechi ya Yanga na Azam, Pele alisema ina
ubora sawa na ligi nyingine kubwa Afrika na akasema sasa kinachotakiwa ni
kuongeza maboresho.
Kuhusu
wachezaji, kulingana na alivyoona mechi ya juzi, Pele alisema kwamba wana uwezo
sawa na wachezaji wengi duniani na ili watimize ndoto za kucheza Ulaya,
wanatakiwa kuongeza juhudi
Aidha, mkali
huyo wa zamani wa mabo wa Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa, aliwaambia
wachezaji chipukizi wa Tanzania kwamba, hakuna njia ya mkato katika kutafuta
mafanikio na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto zao, ikiwa ni pamoja
na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu kucheza fainali za Afrika mwakani.
Pele, ambaye
aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao
dhidi ya AC Milan ya Italia, alisema hayo juzi asubuhi wakati alipotembelea Kituo
cha ufundi cha Karume kushuhudia programu ya mazoezi ya vijana wadogo
inayofanyika kila misho wa wiki kwenye Uwanja wa Karume ambako watoto wa
kuanzia umri wa miaka sita hadi 17 hufundishwa mbinu za kusakata soka.
"Katika
kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye ameletwa
nchini na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuangalia shughuli mbalimbali
za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
"Tunaona
wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze
kucheza kwa kiwango cha juu. Bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria
huwezi kufanikiwa.
"Wale
wenye vipaji vikubwa, lakini hawafanyi jitihada watabakia I. Wale wasiojaliwa
kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata
mafanikio," alisema nyota huyo ww Ghana ambaye alijijengea jina kwa
kufunga mabao safi na muhimu kwa nchi yake na klabu ya Olympique Marseille
wakati ikitamba katika soka barani Ulaya.
"Soka
barani Afrika Lina mazingira yanayofanana. Hakuna motto wa waziri anayecheza
soka. Wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi ww benki ambaye anacheza soka.
Soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia ambazo hazina maisha mazuri na
hivyo man nafasi sawa na wengine wote. Mnachotakiwa kufanya ni kujituma,
kudhamiria na kufanya jitihada ili mfungue mlango wa mafanikio.
Pele, ambaye
watoto wake wainaichezea Marseille, pia aliwataka wachezaji wa timu ya Taifa ya
Vijana walio na umri china ya miaka 17 kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza
fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Algeria mapema mwakani.
"Mkifuzu
mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu," alisema gwiji huyo
ambaye anaiwakilisha FIFA katika kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo.
"Nikiwaangalia naona mna uwezo wa kuwaondoa wapinzani wenu na nitafuatilia
mechi yenu. Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono.
Pele, ambaye
kwa sasa anamiliki shule ya mpira wa miguu ambayo imeshanikiwa kutwaa Kombe la
FA mara moja, ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA kwa nchini za
Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na mmoja wa viongozi wa Idara ya Mawasiano
ya FIFA, Emmanuel Maradas, atakuwa nchini kwa siku tatu ambazo atazitumia
kupata taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo za soka la watoto
(grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi mingine ya maendeleo.