Kapombe mazoezini leo, akiwa mbele ya
John Bocco
|
Na Mwandishi wetu, Kampala
KOCHA wa Tanzania
Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amepata ahueni baada ya beki Shomary
Kapombe kufanya mazoezi leo, kujiandaa na mechi ya kesho dhidi ya Somalia
ambayo itakuwa ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati, CECAFA Tusker Challenge.
Kocha
Poulsen amesema amefarajika mno kurejea kwa beki huyo wa kati wa Simba SC, ambaye
aliumia katika mechi dhidi ya Burundi juzi.
Daktari wa Stars,
Dk Mwanandi Mwankemwa, amesema mchezaji mwingine majeruhi, Mwinyi Kazimoto
hataweza kucheza kwa kuwa bado anaendelea kupata nafuu kwa hivyo wamemshauri
kocha ampumzishe katika mechi ya kesho.
Kocha huyo
Mdenmark, amesema kwamba mechi ya kesho itakuwa ni ya kufa na kupona na kikosi
chake kiko tayari kukamilisha kazi.
Kocha huyo
aliyasema hayo wakati Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanajro Premium
Lager, ikifanya mazoezi ya mwisho leo kabla ya mchezo wake na Somalia ili
kukamilisha michezo ya Kundi B inayojumuisha Burundi, Tanzania, Somalia na
Sudan.
“Mechi hii
ni sawa na kuwa na risasi moja na risasi hii unatakiwa kuitumia vizuri..ndio
mtihani tunaokabiliwa nao katika mechi hii maana lazima tushinde ili tusinonge
mbele katika mashindano haya,” alisema n akikosi chake kitapambana hadi dakika
ya mwisho.
Alisema ana
imani na kikosi chake kwani wachezaji wote wana ari ya ushindi na kuendelea na
mashindano kwani wameshaonesha kiwango kikubwa katika mechi mbili zilizopita
huku Stars ikishinda mechi moja shidi ya Sudan na kufungwa nyingine na Burundi.
“Katika mechi hii hakuna mchezo na
nimeshawaambia wachezaji kabisa maana hapa ukifungwa unaondoka,” alisema.
Meneja wa
Bia ya Kilimanajro Premium Lager, George Kavishe alisema mechi hii ni muhimu
kwa Stars na kuwaomba watanzania wanaoishi Kampala kujitokeza kwa wingi
kuishangilia.
“Vijana hawa wanahitaji sapoti kutoka kwa
wadau wote hasa katika mechi hii ya
kesho itakayoamua kama Tanzania itafuzuu kuendelea au la….sisi tukiwa wadhamini
wa timu tunafuatilia kwa karibu na tunawaomba Tanzania waishangilie na kuipa
moyo timu yao,” alisema.
Kikosi
kinachotarajiwa kuanza katika mchezo huu dhidi ya Somalia ni Juma Kaseja,
Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Frank Domayo,
Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, John Bocco, Shaban Nditi na Salum Abubakary. Beki Amir
Maftah hatacheza kwa sababu ana kadi mbili za njano.