Bridgit katikati akiwa na washindi wake wa pili na wa tatu baada ya shindano usiku huu |
Na Princess Asia
KIMWANA
Bridgit Alfred mwenye umri wa miaka 18, amefanikiwa kutwaa taji la Miss
Tanzania 2012 usiku huu katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Blue
Pearl Hotel, uliopo ndani ya jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Kwa ushindi
huo, kimwana huyo kutoka Kinondoni, Dar es Salaam katika kitongoji cha Sinza, amezawadiwa
Sh. Milioni 8 na gari ambalo aina yake na thamani yake vitajulikana baadaye.
Mshindi wa
pili Euegene Fabian anapewa Sh. Milioni 6.2 na wa tatu Eddah Sylvester anapaewa
Milioni 4.
Washijdi wengine,
wa nne Milioni 3, wa tano Milioni 2.4 na wa sita hadi 15 kila mmoja atapata
Milioni 1.2, wakati washiriki wengine kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh.
700,000.
Mapema mwaka
huu, Kamati hiyo iliendesha shindano dogo na kumpata Lissa Jensen ambaye
aliwakilisha nchi katika fainali za Dunia kutokana na mabadiliko ya kalenda
yaliyofanywa na Kamati ya Miss World na mrembo atakayetwaa taji hilo katika
fainali hizo zitakazofanyika hivi karibuni atapata muda mrefu wa kufanya
maandalizi.
Shindano la
Miss Tanzania lilianza rasmi mwaka 1994 na Aina Maeda alikuwa mshindi wa
kwanza, akifuatiwa na Shose Senare 1995, Emily Adolf 1996, Saida Kessy 1997,
Basila Mwanukuzi 1998, Hoyce Temu 1999, Jacqueline Ntuyabaliwe 2000, Happiness
Magese 2001, Angela Damas 2002, Sylvia Bahame 2003, Faraja Kotta 2004, Nancy
Sumary 2005, Wema Sepetu 2006, Richa Adhia 2007, Nasreem Kareem 2008, Miriam
Gerald 2009, Geneveive Mpangala 2010 na Salha Israel 2011.
Awali ya
hapo, mwaka 1967 lilifanyika shindano la kwanza kabisa la Miss Tanzania na Theresa
Shayo akashinda katika shindano lililofanyika kwenye bwawa la kuogelea la
hoteli ya Kilimanjaro, lakini serikali ya Tanzania wakati huo, chini ya rais wa
kwanza, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikapiga marufuku mashindano kwa
sababu hayaendani na mila na desturi za Mtanzania.
Lakini Lino
International Agency, ikajenga hoja ambazo ziliishawishi serikali ya Tanzania,
chini ya rais wake wa pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kuruhusu mashindano hayo
yafanyike tena, ingawa mwaka 2001 yaliponea chupuchupu kufutwa tena, enzi za
rais wa awamu wa tatu, Benjamin William Mkapa.
Ilitokana na
vazi la kuogelea ‘kichupi’, ambalo lilipingwa kwa sababu linamdhalilisha
mwanamke wa Tanzania, lakini Lino ikaboresha kipengele cha vazi hilo, kutoka la
kuogelea hadi la ufukweni, ambalo kidogo linamsitiri binti na serikali
ikaruhusu mashindano yaendelee.
Hata hivyo,
mabinti wanapokwenda kwenye shindano la dunia, wanavaa vazi la kuogelea kupanda
jukwaani, katika shindano ambalo linaonyeshwa moja kwa moja nchi zaidi ya 100
duniani na picha zao kuchapishwa kwenye majarida, magazeti na mitandao
mbalimbali duniani.
Bridgit sasa
atashiriki shindano la Miss World mwakani, baada ya Lisa kushiriki mwaka huu na
kuanzia sasa atakuwa akiandaliwa kwa ajili ya fainali hizo.