Washiriki wa EBSS Salma Yussuf Abushir,
Nsami Nkwabi, NshomaNghangasamala, Walter Chilambo na Wababa Mtuka wakiwa na
Ritha Poulsen. Je, nani ataondoka na kitita cha Sh. Milioni 50 kesho?
|
Na Prince Akbar
BAADA ya miezi mitatu ya mchuano mkali hatimaye mshindi wa
shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search atapatikana leo katika fainali
kali inayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Mshindi atajinyakulia shilingi milioni hamsini pamoja na
mkataba wa kurekodi kutoka kwa wadhamini pekee wa shindano hilo kampuni ya simu
za mikononi ya Zantel.
Washiriki walioingia kwenye fainali hizo ni EBSS06: Nsami
Nkwabi, EBSS07: Nshoma Ng’hangasamala, EBSS09: Salma Abushiri, EBSS11: Wababa
Mtuka (Dar) na EBSS12: Walter Chilambo (Dar).
Wasanii watakaoburudisha ni Rich Mavoko, Omi Dimpoz, Ben
Paul, Lina, Amini, Mzee Yusuf, Haji Ramadhan, Mwasiti, Ditto, Laila Rashid,
Linex na Barnaba.
Akizungumzia fainali hizo, jaji mkuu wa shindano hilo, Madam
Ritha Paulsen, aliwashukuru watanzania kwa ushirikiano waliowapa toka shindano
limeanza mpaka leo wanahitimisha kwa fainali.
‘Kama mlivyoona
shindano hili toka lilipoanza mwaka huu limekuwa la kimataifa zaidi, hivyo
tarajieni fainali za kipekee na zitakazoweka rekodi kwenye tasnia ya burudani
na ni matarajio yetu kwamba mshindi wa usiku huu atafanya vizuri kwenye muziki’
alisema Madam Ritha.
Kwa upande wake Afsa Biashara mkuu wa Zantel, bwana Sajid
Khan alisisitiza utayari wa kampuni yake katika kuwaendeleza vijana wa
kitanzania kufikia ndoto zao lakini aliomba pia wadau wengine wa sanaa kuwapa
washirikiano washiriki wote.
‘Zantel, pamoja na kumpa mshindi zawadi ya milioni hamsini
lakini pia tutampa mkataba wa kurekodi, na washiriki wengine watapewa nafasi ya
kurekodi wimbo mmoja mmoja lakini juhudi hizi zitafanikiwa ikiwa tutapata
ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau’ alisema Khan.
Shindano hilo limekuwa likirushwa hewani na kituo cha runinga
cha ITV, lilianza mwezi wa sita kwa kufanya usaili mikoani, ambalo mwaka huu
lilienda mikoa nane-Mbeya, Dodoma, Mwanza, Tanga, Dar es Salaam, Zanzibar,
Lindi pamoja na Arusha.
Kwa mara ya kwanza pia shindano hilo liliweza kufanya usaili
kwa njia ya simu ili kuwapa nafasi vijana zaidi ambao hawakufikiwa na majaji.
Epiq Bongo Star Search ni kipindi cha televisheni ambacho
huibua vipaji vya muziki kwa vijana wa kitanzania na kinatengenezwa na Benchmark
Productions, na toka kimeanzishwa mwaka 2006 kimekuwa ni kipindi kinachotazamwa
zaidi Afrika mashariki kwa kufikisha watu milioni 3 wanaotazama kwa kila
kipindi.
Mwaka huu kinadhaminiwa na kampuni ya simu za mikononi ya
Zantel, na mshindi atapata zawadi ya shilingi milioni 50 pamoja na mkataba wa
kurekodi.