Profesa Milovan Cirkovick |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA wa
Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick anaweza kutimuliwa wakati wowote kwenye
klabu hiyo, kufuatia kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo.
Uongozi wa
Simba unamtuhumu Mserbia huyo kwamba ni mbishi hashauriki na hilo limekuwa likiigharimu
timu katika michezo yake ya karibuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
“Huyu jamaa
tumemvumilia sana, mimi sina hamu naye tena, sijui wenzangu. Anapanga kikosi ovyo
na ndiyo chanzo cha matokeo haya mabaya,”alisema kiongozi mmoja wa Simba.
Lakini kwa
upande mwingine, inadaiwa matokeo haya mabaya ya Simba ni matokeo ya mgomo wa
wachezaji wakishinikiza wachezaji wenzao waliosimamishwa Haruna Moshi ‘Boban’
na Juma Nyosso warejeshwe kikosini.
Zaidi Boban,
wachezaji wanadaiwa kumpenda sana kutokana na roho yake safi ya kibinadamu na
upendo mkubwa kwa wenzake.
Boban ndiye
mchezaji pekee aliyejitolea kuusindikiza nyumbani kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC) mwili wa marehemu Patrick Muteesa Mafisango, kiungo wa Simba aliyefariki
dunia Mei mwaka huu kwa ajali ya gari.
Simba SC
jana ilifungwa mechi ya kwanza ya Ligi Kuu mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro, mabao ya Said
Mkopo na Hussein Javu.
Simba
inabaki na pointi zake 23, baada ya kucheza mechi 12, ikiipisha kileleni Yanga
yenye pointi 26 sasa. Simba itamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kumenyana
na Toto African uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.