Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mkuu wa
timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Mdenmark Jacob
Michelsen amesema kwamba kuelekea mechi ya keshokutwa ana wasiwasi wapinzani wake,
Kongo Brazzaville wana wachezaji waliozidi umri.
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mazoezi ya jioni,
Michelsen alisema kwamba ameichunguza vizuri Kongo na sasa anaifahahamu vema.
Serengeti itamenyana
na Kongo keshokutwa Uwanja wa Taifa, katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Tatu na
ya mwisho ya kuwania kucheza Fainali za Vijana Afrika zitakazofanyika nchini
Morocco mwakani.
Michelsen alisema
kwamba alikwenda kushuhudia mchezo wa kwanza wa raundi iliyopita, baina ya
Kongo na Zimbabwe waliotolewa na wapinzani wao hao na kujionea makali ya
wapinzani wao.
Pamoja na
kukiri kwamba Kongo ni timu bora na ilicheza Fainali zilizopita za Kombe la
Dunia nchini Mexico mwaka jana na kutolewa raundi ya pili, Michelsen alisema
bado ana wasiwasi timu hiyo ina ‘vijeba’.
“Nilipokwenda
kuwaangalia wakicheza na Zimbabwe, nilikuta kikosini mwao kuna wachezaji sita
wa kikosi kilichokwenda Mexico kwenye Kombe la Dunia, inanitia shaka kwa sababu
hakuna mchezaji anayeweza kucheza michuano mikubwa kama ile akiwa ana umri wa
miaka 15.
Mimi ni
kocha wa vijana na ninajua, haiwezekani. Ucheze fainali za Kombe la Dunia za U17
una miaka 15, hakuna,”alisema Michelsen, ambaye aliwataja baadhi ya wachezaji
anaowatilia shaka wamezidi umri ni Hady Binguila na Charvely Mabiat.
Pamoja na
hayo, Michelsen amesema ana matumaini ya kuwatoa Kongo kutokana na maandalizi
yao ya muda mrefu na pia sapoti anayoipata kutoka kwa viongozi wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) na Kamati maalum iliyoundwa kuhakikisha timu hiyo inafanya
vizuri.
Amesema wamecheza
mechi za kujipima nguvu 15 zikiwemo dhidi ya timu za Ligi Kuu na hawajafungwa
hata moja, kitu ambacho anaamini ni kipimo cha ubora wa timu yake.
Kwa upande wake,
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Serengeti Ishinde, Kassim Dewji alisema
kwamba wanapambana kwa uwezo wao wote kuhakikisha timu hiyo inakwenda kwenye
fainali za Morocco, mwakani.
Dewji aliwataka
wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa nidhamu, kujituma na kufuata maelekezo ya
makocha wao, ili wapate ushindi katika mchezo wa Jumapili.
Serengeti
imefanikiwa kufuzu hadi Raundi ya Tatu bila jasho, baada ya wapinzani wake wa
awali katika Raundi ya Kwanza na ya Pili, Kenya na Misri kujitoa. Iwapo timu hii
itafuzu, hii itakuwa mara ya pili kwa Serengeti kukata tiketi ya kucheza
fainali hizo, baada ya mwaka 2005.
Hata hivyo,
pamoja na kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, Serengeti haikwenda Gambia mwaka
huo kutokana na kuondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF),
baada ya kubainika walitumia kijana aliyezidi umri, Nurdin Bakari.