Mussa Mgosi |
Na Mahmoud Zubeiry
MUSSA Hassan
Mgosi ameondoka jana kwenda China kucheza soka ya kulipwa, akichukua nafasi ya
Said Bahanuzi, ambaye klabu yake, Yanga imemzuia.
Habari ambazo
BIN
ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Mgosi ambaye amesajiliwa JKT Ruvu ya
Pwani msimu huu, akitokea DC Motemba Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), ameondoka na wachezaji wengine wawili wa ‘mchangani.
“Baada ya
Yanga kuwazuia Cannavaro (Nadir Haroub) na Bahanuzi, nafasi zao wamechukua
Mgosi na vijana wengine wawili, mmoja kipa na mwingine beki, kutoka mchangani
tu, lakini wanajua sana,”kilisema chanzo cha habari.
Mgosi hakucheza
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kutokana na kukosa hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) kutoka DRC.
Cannavaro na
Bahanuzi waliotarajiwa kuondoka juzi saa 10:00 jioni kwa ndege ya Qatar Airways
kwenda China, kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa, walizuiwa na klabua
yao.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb aliiambia BIN
ZUBEIRY kwamba, sababu za kuzuiwa kwa wachezaji hao ni kutokana na
klabu inayowataka kutofuata taratibu.
“Hawajatuma
barua, hawa wanataka kwenda kienyeji tu, na sisi si kama tumewazuia, tumeitaka
kwanza hiyo klabu ifuate taratibu kwa kutuma barua huku na kujitambulisha, ili
hata hao wachezaji wakipata matatizo tujue tunaanzia wapi,”alisema Bin aKleb.
Mapema wiki
hii, Cannavaro, Nahodha Msaidizi wa Yanga aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba wanakwenda
China kwa wiki mbili na baada ya majaribio kama wakifuzu, klabu inayowataka
itafanya mazungumzo na klabu yao.
“Sisi wote
tuna mikataba na klabu, hivyo tukifuzu jamaa itabidi watuhamishe
Yanga,”alisema beki huyo kati
aliyezaliwa Februari 10, mwaka 1982.
Cannavaro
yupo Yanga tangu mwaka 2006, aliposajiliwa kutoka Malindi ya Zanzibar wakati
Bahanuzi amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwaka 2009,
Cannavaro alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada na
baada ya miezi sita alirejeshwa Yanga alikoendelea kucheza hadi leo anakwenda
kujaribu bahati yake China.
Bahanuzi
ameingia na zali la aina yake Yanga SC, kwani katika mashindano ya kwanza
kuichezea klabu hiyo alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na kati, Kombe la Kagame.
Hadi sasa, Said
Bahanuzi maarufu kama Spider Man,
ameifungia Yanga mabao 12 katika mechi 14, yakiwemo matatau ya penalti tangu
ajiunge na timu hiyo Julai mwaka huu.
Kwa sasa China ni nchi ambayo mastaa wengi waliokuwa Ulaya
wanakwenda kumalizia soka yao, mfano washambuliaji wawili wa zamani wa Cheslea,
Didier Drogba na Nicolas Anelka waliopo Shenghua Shanghai. Anelka ni kocha
mchezaji.