SOKA ya Tanzania imechafuka tena kwa tuhuma chafu za hongo
katika mchezo, ambazo zimewaponza wachezaji wanne wa klabu ya Ligi Kuu, Azam
FC, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kupoteza
ajira zao.
Na Mahmoud Zubeiry
|
Nasema kupoteza ajira zao, kwa sababu baada ya kuwasimamisha,
viongozi wa Azam wamesema hawawahitaji tena wachezaji hao katika timu yao na
mwakani watakisuka upya kikosi chao.
Nani atasajili wachezaji wauza mechi kati ya timu kubwa za
Tanzania, ina maana hao ndio mustakabali wao kisoka umeharibika.
Dida, Nyoni na Morris wote hawa ni wachezaji wa Taifa Stars,
tena tangu enzi za Mbrazil Marcio Maximo tazama hasara tunayoelekea kuipata na
inauma zaidi kwa nafasi ya beki ya kati, ambayo wachezaji wake wamekuwa adimu
nchi hii kwa miaka ya karibuni.
Bado najiuliza, ni kweli wachezaji hawa walihujumu timu yao,
ama ni dhana tu au wamefitiniwa?
Soka ya nchi hii inakwamishwa na mambo mengi sana, lakini
kubwa ni uelewa mdogo wa wengi kati ya viongozi wetu, ambao wanaingilika kwa
urahisi mno kimajungu na fitina. Nina wasiwasi kwamba inawezekana wachezaji
hawa wamefitiniwa, lakini pia siwezi kubisha juu ya tuhuma hizi kwa sababu haya
mambo yapo.
Kumbuka, Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, mwaka
huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu na baada ya hapo
ikamfukuza kocha wake Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart
Hall.
Bunjak alifukuzwa kwa sababu ya kushuka kwa uwezo kwa timu
kwa kipindi alichokuwa kazini, kwa mujibu wa Azam wenyewe, lakini kumbe
wachezaji walikuwa wanamsaliti kwa mujibu wa Azam pia.
Ndiyo, alifungwa mechi moja tu kwenye Ligi Kuu, hiyo ya 3-1
na Simba na baada ya hapo akafukuzwa, baadaye inakuja kujulikana wachezaji
walipewa fedha wahujumu timu. Tazama mkanganyiko huu.
Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata
taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi kwa kushirikisha hadi na Taasisi ya
kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo ilipokamilisha uchunguzi wake
wakatoa ripoti inayowataja wachezaji hao wanne kupokea rushwa kutoka kwa kiongozi
mmoja wa Simba.
Wachezaji tumewajua, tumewajua kutokana na taarifa za wenyewe
Azam, lakini huyu kiongozi ni nani na kwa nini naye asitajwe?
Azam inadhani imewatendea haki kuwatangaza wachezaji hawa
kuhusika na tuhuma hii nzito, bila ya kumtaja mtuhumiwa mwingine, ambaye haswa
ndiye kirusi, huyo aliyewahonga?
Bado nakumbuka Dida hakucheza mechi hiyo, kwani Oktoba 27,
kikosi cha Azam kilikuwa;
Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris,
Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha
Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre
Herman Tcheche na Salum Abubakar.
Siku hiyo,
Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka
beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba
Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa
krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi
aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni
mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na
dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini
mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka
mabeki wa Azam.
Hivyo basi,
Dida hata kama alipokea hongo aliitumikiaje na si yeye aliyesimama langoni?
Hapo hapo,
tunaambiwa TAKUKURU imefanyia kazi suala hilo, tunafahamu kwa mujibu wa sheria
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania rushwa ni kosa la jinai, na je nini
kinachofuata sasa baada ya kuwatia hatiani wachezaji na huyo kiongozi wa Simba?
Huku kwetu
kwenye mpira rushwa haitakiwi kabisa na kushiriki au kuhusika kwa namna yoyote
katika kashfa hiyo ni ukosefu wa uadilifu na soka haihitaji kiongozi wala
mchezaji asiye mwadilifu.
Pamoja na
hayo, kwa muda mrefu tu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeendelea kukaa
kimya kabisa.
Nakumbuka
sakata la Shaaban Kado na Ulimboka Mwakingwe Morogoro mwaka juzi na bado kuna
mambo mengi tu mengine tu yanazungumzwa, lakini TFF ipo kimya kana kwamba nayo
inasapoti mchezo mchafu katika soka yetu.
Wakati
mwingine maneno yanazungumzwa kwamba kuna baadhi ya klabu zinahonga hadi
maofisa wa TFF ili wawekewe mambo fulani fulani kwa matakwa yao, mfano
kupangiwa marefa wanaowataka na aina ya ratiba wanayotaka wao.
Soka yetu
imechafuka kwa kweli. Tukirejea kwenye sakata la Azam, klabu hiyo izingatie ina
mikataba na wachezaji hao na iliwasajili kwa fedha na bila shaka walikuwa
kwenye mipango yao ya muda mrefu.
Je,
kuwafukuza tu ni dawa na pia ni kuwatendea haki? Bado sioni kama tunakaribia
hata robo ya suluhisho la tatizo hili.
Hapo juu
nimesema, Bunjak alifukuzwa kwa sababu ya madai ya kushuka kwa kiwango cha
timu, lakini kumbe wachezaji walimhujumu! Na hapa klabu imepata hasara kwa
kuvunja mkataba na kocha na kumlipa fedha nyingi, kisha kuajiri kocha mwingine.
Maana yake,
hasara hii imeletwa na hawa wachezaji walioufanya uongozi uamini Bunjak si
kocha mzuri. Tazama jinsi ambavyo sakata hili linavyozalisha maswali mengi
yasiyo na majibu. Hiyo ndio soka ya
bongoi!