MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unaelekea ukingoni, huku Top Three ile ile (Simba,
Yanga na Azam) iliyotarajiwa ikichuana kileleni kuwania ubingwa.
Na Mahmoud Zubeiry |
Shukrani kwao Coastal
Union ya Tanga iliyoongeza ushindani katika Ligi Kuu msimu huu, kwani tangu
mwanzo imeonyesha kula sahani moja na Farasi hao watatu wanaofukuzia ubingwa.
Lakini wakati Ligi Kuu
ikielekea ukingoni, tayari kuna malalamiko ya timu hizo zinazofukuzana kuwania
ubingwa kuhonga marefa na timu pinzani.
Na utamu unakuja kwamba,
ni timu hizo hizo zenyewe kwa zenywe ndizo zinazolalamikiana. Viongozi wa Simba
wanalalamika Yanga inanunua mechi na marefa. Viongozi wa Yanga wanalalamika
Simba inanunua mechi na marefa.
Simba na Yanga pia
wanailalamikia Azam inanunua mechi na marefa na ndiyo maana msimu huu kabla ya
kumenyana na timu hiyo, zote zimekwenda kuweka kambi nje ya mji.
Simba walikwenda Zanzibar
wakidai wanawaweka wachezaji wao mbali na mazingira ya kurubuniwa, hali kadhalika
na Yanga leo wataingia Uwanja wa Taifa, kumenyana na Azam wakitokea Bagamoyo
mkoani Pwani, kwa madai kama hayo.
Kwa kweli inasikitisha
sana soka yetu inapoelekea, kwani pamoja na kucheza ligi ili tupate bingwa,
lakini ligi yetu kama ilivyo ligi za nchi nyingine zote barani Afrika,
inachezwa kutafuta wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya Afrika.
Namaanisha Ligi ya
Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) na kwa mwakani Tanzania tutawakilishwa
na Simba na Azam kwenye michuano hiyo.
Inasikitisha katika
kipindi cha miaka 50 ya uhuru wetu, Tanzania haijawahi kutwaa taji hata moja la
michuano hiyo ya mikubwa Afrika, zaidi tu ya kufika fainali mara moja, mwaka
1993.
Ni klabu moja tu ambayo
tunaweza kusema imekuwa ikijitutumua kwenye michuano ya Afrika, Simba SC na
ndiyo iliyofika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa na Stella
Abidjan mabao 2-0 mjini Dar es Salaam, licha ya kuanza vyema kwa sare ya bila
kufungana ugenini.
Ni hao Simba walifika Nusu
Fainali ya Klabu Bingwa Afrika pia mwaka 1974 na kutolewa na Mehallal El Kubra
ya Misri.
Kabla ya hapo, Yanga SC ya
Dar es Salaam ilicheza Robo Fainali ya michuano hiyo mara mbili mfululizo mwaka
1969 na 1970, mara zote ikitolewa na Asante Kotoko ya Ghana.
Hatua nzuri na za mwisho
kwa klabu zetu kufikia kwenye michuano ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi,
au nane bora michuano hiyo, Yanga 1998 na Simba 2003.
Kila mwaka timu zetu
zinapotolewa yanaonekana makosa ya wazi ambayo miaka nenda rudi yamekuwa
hayafanyiwi marekebisho, matokeo yake desturi imeendelea kuwa ile ile, timu
zetu kuboronga kwenye michuano ya Afrika.
Inasikitisha, hasa
tukirejea historia ya klabu zetu kongwe nchini, Simba na Yanga zilianza vizuri
na wengi walitarajiwa zitakuwa tishio kutokana na mafanikio yake ya miaka ya
1970.
Klabu zetu zilikuwa
hazitishwi na klabu za nchi jirani hata Zambia, Kenya au Uganda kwenye michuano
ya Afrika, lakini hali ikoje leo?
Ni msiba mzito iwapo
ratiba ya michuano ya Afrika itatoka na Simba au Azam ikapangiwa kucheza na
timu kutoka Zambia; maana yake ni safari tu.
Tatizo nini? Hilo ndilo
jambo ambalo umewadia wakati sasa tujiulize, kwani starehe ya mashabiki wa soka
ni ushindi na mataji, je, Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikishiriki michuano
ya Afrika karibu kila mwaka, je zinakata kiu hiyo?
Na kama hazikati kiu hiyo
ya mashabiki wao, tatizo ni nini?
Tanzania tuna tatizo kubwa
na la msingi, kukosa viongozi weledi wenye dira. Hakika hilo linaitafuna haswa
soka yetu.
Na mbaya zaidi viongozi wa
soka wa nchi hii wanajifanya wajuaji, hawashauriki, hawaambiliki, wakati
wengine ukiwaambia wakutajie sheria tano tu kati ya 17 za soka hawawezi.
Hawajui soka wanakuja
kwenye soka kutibu njaa zao na matokeo yake soka yetu inazidi kudidimia. Tazama
DRFA (Chama cha Soka Dar es Salaam), kuna watu wamejitokeza kugombea uongozi,
yaani sura zao zinanuka njaa ya fedha kwa sababu wanajua pale kuna fedha nyingi
inaingia.
Hawaonyeshi dalili za
kwenda DRFA ili kufanya kazi ya mpira wa miguu, bali wanakwenda kutaka kufanya
ufisadi huo. Ukiwasikiliza maneno yao tu kila siku, unajua hawa ni ‘wazee wa
njaa’, wamejawa na tamaa ya fedha hadi mtu unaingiwa hofu juu yao.
Na hata hao wenye kuijua soka
kwa maana ya kuanzia kwenye kuicheza, wengi wao wameangukia kwenye dimbwi la
tamaa na kujilimbikizia mali, kwa kunyonya jasho la wachezaji. Soka yetu
itaenda wapi?
Viongozi wetu wanapaswa
kuelewa, jambo lolote linalofana, linatokana na maandalizi mazuri.
Hata nchi yetu iliyotimiza
miaka 50 ya Uhuru, ili kuupata huo uhuru, yalifanyika maandalizi ya kupanga
mikakati juu ya namna ya kuudai hadi Muingereza akakubali kutuachia taifa letu.
Hakukurupuka Mwalimu
Nyerere (marehemu) na viongozi wenzake wa TANU kwenda kudai Uhuru, walijipanga
na ndiyo maana tuliupata uhuru wetu pasipo kudondosha tone la damu.
Sasa kuelekea kwenye
michuano ya Afrika mwakani kwa mfano, baada ya mzunguko wa kwanza utasikia
wawakilishi wetu wanafanya usajili wa kishindo kama wa mwanzo wa msimu vile.
Si tayari tumesikia Simba
wamekwishawapigia mstari mwekundu wachezaji wao kadhaa wakiwemo Komal Bil Keita
kutoka Mali na Daniel Akufo kutoka Ghana, huku Juma Nyosso na Haruna Moshi
taarifa za ndani zikisema hawatarudishwa tena baada ya kusimamishwa-
kinachofuata ni nini?
Ili tufanikiwe katika
soka, tunapaswa kuwa na mipango, tena ya muda mfupi, kati na mrefu
iliyotengenezwa na wataalamu. Kabla ya kuingia kwenye michuano ya Afrika, Simba
na Azam zinapaswa kuwa na maandalizi ya uhakika yanayotokana programu za
makocha wao na si kwenda hobela hobela, leo Kombe la Mapinduzi, kesho mechi ya
kirafiki ya kuganga njaa. Hapana.
Viongozi wetu wanachojua
wao kusajili tu wachezaji wapya kila unapowadia muda wa kusajili, hawajui
kwamba wanatakiwa kutengeneza timu kwa kuiandaa.
Timu zetu hazitaki
kufungwa na ndiyo maana hata zinaibuka hizi tuhuma za kununua mechi. Katika
soka kufungwa ni jambo la kawaida kama ilivyo kutoa sare au kushinda, mbaya ni
timu yako kuwa ya kufungwa kila siku, hiyo si timu ya ushindani.
Na dawa ya kufungwa si
kusajili jamani, ni kuangalia mapungufu ya timu na ya kuyafanyia kazi.
Tazama Arsenal msimu uliopita
wa Ligi Kuu ya England walianza kwa kusuasua hadi kufikia kufungwa mabao 8-0 na
Manchester United, lakini baadaye wakaimarika, kufuatia kufanyia kazi mapungufu
yao.
Babu Arsene Wenger
aliifanyia tathmini timu yake akagundua mapungufu yake akaanza kuyafanyia kazi
na timu yake ikawa imara, tena na kushindana na timu zilizofanya usajili wa
kufuru.
Kichekesho usajili wenyewe
unaofanywa na Simba na Yanga hauna tija. Mchezaji mpya anasajiliwa ili kuongeza
nguvu kwenye kikosi, lakini kwa klabu zetu wengine sijui wanasajili shemeji
zao, maana mtu mpya anasajiliwa halafu hata jezi havai
Kuna tatizo, wengi
wanaingia kwenye uongozi wa soka kwa maslahi yao binafsi na si kwa nia ya dhati
ya kuitumikia soka ya nchi hii. Fedha za milangoni zinawafanya wapiganie
uongozi wa klabu wakajichotee na wenyewe wana msemo wao, eti; “Hela ya mpira
haina mwenyewe, na hafungwi mtu akiiba”.
Sawa, waibe lakini basi
wajifunze kula na vipofu kwa kuziandaa timu vizuri ili zifanye vizuri kwenye
michuano mikubwa. Lakini pia michuano hiyo ina fedha nyingi pia kuanzia za
milangoni hadi zawadi, hivyo wakiandaa timu vizuri zikawa za ushindani watavuna
zaidi. Hawajui hilo?
Kwa kuwa wanashindwa
kuandaa timu vizuri baada ya kufanya usajili, matokeo yake hata mechi
wanazoshinda wanatuhumiwa kununua. Kuna faida gani kusajili wachezaji kwa
mamilioni ya shilingi halafu kesho unanunua mechi?
Umeleta Kocha Mzungu
unamlipa kwa fedha ya kigeni, anaishi kwa gharama kubwa, maana yake huyu ni
mtaalamu atusaidie kukuza yetu, lakini badala yake sasa kazi yake unaifanya
wewe kwa kununua mechi.
Hebu sasa wakati umefika na
tujiulize mara mbili mbili, mchezo huu utatufikisha wapi na kwa nini sasa
tusiachane nao? Jumapili njema.