Athumani Bilal |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA aliyeiongoza
Toto Africans kuifunga Simba SC 1-0 katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Athumani Bilal ameomba wadau wa mkoa wa Mwanza
wamsaidie kumsomesha kozi za ukocha, ili aendeleze kipaji chake hicho.
Bilal
aliiongoza Toto katika mchezo huo wa juzi, kwa sababu bosi wake, John Tegete yuko
kwenye maandalizi ya mchezo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya
Kenya mjini Mwanza.
“Naomba
msaada mdau yeyote ajitokeza kunisomesha kozi ya juu ya ukocha, popote, hata
ndani au nje ya nchi, kwa sababu nahitaji kuboresha taaluma yangu,”alisema kiungo
huyo wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza ‘TP Lindanda’.
Bilal ameomba
hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limfikirie kwa sababu akipata taaluma
nzuri anaweza kuja kulisaidia hata taifa siku za baadaye.
“Nadhani
nimewaonyesha watu uwezo wangu hadi sasa na wameona jinsi ambavyo Toto ilicheza
mpira mzuri dhidi ya Simba hadi tukafanikiwa kushinda, kwa hivyo naomba wanisaidie
kujiendeleza,”alisema.
Bao pekee la
Mussa Said Kimbu dakika ya 73, juzi liliizamisha Simba SC kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Kimbu
alifunga bao hilo akiunganisha krosi ya Mganda, Mohamed Jingo tena akipitisha
mpira katikati ya msitu wa mabeki wa Simba na kipa wao, Wilbert Mweta.
Simba
hawakucheza vizuri kama timu siku hiyo, ila kwa mchezaji mmoja mmoja, karibu
kila mchezaji alicheza vizuri na Emanuel Okwi ndiye aliyekuwa akiisumbua zaidi
ngome ya Toto.