Shikanda |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
muda wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, James Nandwa amesikitika
kumkosa beki wa Azam FC ya Tanzania, Ibrahim Shikanda katika Kombe la Mataifa
ya Afrika Mashariki na Kati, Tusker Challenge zinazoendelea mjini hapa.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY katika mahojiano maalum mjini hapa jana, Nandwa anayemshikia
timu hiyo kwa muda Mfaransa Henri Michel, alisema kwamba alimuita Shikanda
katika kikosi chake cha Tusker Challenge, lakini akashindwa kuja kwa sababu ni
majeruhi.
“Nilimuita
Shikanda, lakini akasema yeye ni mgonjwa hawezi kuja, kwa kweli kwangu na kwa
benchi zima la ufundi tumesikitika kumkosa beki mzuri kama Yule, ambaye
anafanya vizuri hadi katika klabu yake,”alisema Nandwa.
Hata hivyo,
kocha huyo alisema kwamba anakubaliana na matokeo na ataendelea na wachezaji
alionao kuhakikisha kwamba anarejea na Kombe Kenya.
“Michuano ni
migumu, hasa kundi letu, kama unavyoona tumefungwa na Uganda, lakini bahati
haikuwa yetu. Tulitengeneza nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia, wenzetu
wametumia nafasi waliyopata.
Na ugumu
zaidi upo kwenye kundi. Hakuna timu dhaifu. Kuna Ethiopia ambao wamefuzu
kucheza Fainali za AFCON (Mataifa ya Afrika). Sudan Kusini umewaona wameisumbua
Ethiopia, hili ni kundi gumu sana,”alisema Nandwa.
Hata hivyo,
amesema watapambana kushinda mechi zao zote zilizosalia ili watinge Robo
Fainali.
Kenya jana
wameanza vibaya CECAFA Tusker Challenge baada ya kuchapwa na Uganda bao 1-0
kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala, Uganda.
Mbaya wao
jana alikuwa ni mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito
aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma
Dennis.
Kwa ushindi
huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi
zake tatu kila timu.
Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote
zilishambuliana kwa zamu.
Kenya
walianza kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake
wachache waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa
raha mashabiki wao kwa soka safi.
Mchezo
uliendelea kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande
wakicheza kwa kujiamini.
Lakini sifa
ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya
juu.
Kipindi cha
pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika saba
baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo,
ndipo kabumbu likaanza tena.
Michuno hiyo
itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye
Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
Uganda; Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma
Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey
Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
Kenya; Duncan Ochieng, Anthony Kimani,
Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David Ochieng, Lama Salim Mohamed,
Bernard Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’ Kimani/Enock Obiero na Clifton
Miheso/Paul Were.