Okwi wa kwanza kulia waliosimama na Kiiza mbele yake aliyeinama akiwa katika kikosi cha Uganda kilichoifunga Kenya jana |
KOCHA Mkuu
wa timu ya soka ya taifa ya Uganda, The Cranes, Bobby Williamson raia wa
Scotland, amesema kwamba wachezaji Hamisi Friday Kiiza na Emmanuel Arnold Okwi
ni tegemeo lake katika kampeni za kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki
na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwaka huu mjini hapa.
Akizungumza
katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY mjini hapa jana, kocha
huyo kipenzi cha Waganda alisema anawategemea sana Okwi na Kiiza kutwaa taji la
pili mfululizo la Tusker Challenge katika fainali za nyumbani.
Alisema
wachezaji hao wamekuwa wakiimarika siku hadi siku na ndiyo maana ameendelea
kuwa nao katika kikosi cha The Cranes tangu ameana nao miaka mitatu iliyopita.
“Kila siku
uwezo wao unazidi kupanda na nadhani wakati au bahati yao ya kucheza Ulaya
haijafika tu, wote ni viwango vya kucheza Ulaya au nchi nyingine kubwa kuliko
kwetu Afrika Mashariki,”alisema.
Aliwasifu
wana nidhamu na ni wazalendo- wana mapenzi na timu yao ya taifa. “Wanajituma
sana nikiwa nao, wana nidhamu na wanapenda nchi yao, nawapenda sana,
wananifurahisha,”alisema.
Bobby
alizipongeza pia klabu zao, Simba (Okwi) na Yanga (Kiiza) zote za Tanzania kwa
kuwatunza na kuwalea vizuri wachezaji hao, ndiyo maana uwezo wao umekuwa
ukipanda siku hadi siku.
“Unajua
mchezaji anatunzwa na klabu, kama klabu haikai vizuri na mchezaji hawezi kuwa
katika kiwango kizuri, na kama hana kiwango kizuri siwezi kumchukua timu ya
taifa. Kwa hivyo hata klabu zao nazishukuru kwa kunilelea vizuri hawa
vijana,”alisema.
Okwi na
Kiiza jana waliiongoza Cranes kuilaza 1-0 Kenya katika mchezo wa ufunguzi wa
Tusker Challenge uliopigwa kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala,
Uganda.
Shukrani
kwake, mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito aliyefunga
bao hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma Dennis.
Kwa ushindi
huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi
zake tatu kila timu.
Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote
zilishambuliana kwa zamu.
Kenya
walianza kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake
wachache waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa
raha mashabiki wao kwa soka safi.
Mchezo
uliendelea kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande
wakicheza kwa kujiamini.
Lakini sifa
ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya
juu.
Kipindi cha
pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika saba
baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo,
ndipo kabumbu likaanza tena.
Michuno hiyo
itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye
Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Uganda kilikuwa; Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma
Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey
Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
Kenya; Duncan Ochieng, Anthony Kimani,
Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David Ochieng, Lama Salim Mohamed,
Bernard Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’ Kimani/Enock Obiero na Clifton
Miheso/Paul Were.