Kocha wa Burundi, Lotfy Mohamed |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
timu ya soka ya taifa ya Burundi, Int’hamba Murugamba, Mmisri Lotfy Mohamed
amesema kwamba amemtema kwenye kikosi chake mshambuliaji wa Yanga SC ya Dar es Salaam,
Didier Kavumbangu kwa sababu hamuhitaji kwenye mipango yake ya sasa.
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY jana mjini hapa, Mohamed alisema kwamba amekuja na kikosi cha
wachezaji ambao wanacheza Ligi ya Burundi pekee na hajachukua mchezaji hata
mmoja anayecheza nje.
Amesema sababu
ya kufanya hivyo ni kuanza kuwaandaa wachezaji wa kucheza michuano ya kuwania
tiketi ya kucheza fainali za CHAN, ambazo huhusisha nyota wanaocheza ligi za
nyumbani kwao pekee.
“Siyo Kavumbangu
tu, kuna wachezaji wengine wazuri tu wanaocheza hadi Ulaya, lakini
sikuwachukua, kwa sababu siwahitaji katika mipango yangu ya sasa, bado ni
wachezaji wa timu ya taifa na naheshimu uwezo wao,”alisema Mohamed.
Kavumbangu alisajiliwa
Agosti mwaka huu Yanga akitokea Atletico ya Burundi, baada ya kung’ara kwenye
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Komnbe la Kagame.
Bila Kavumbangu
na mastaa wengine wa nje, ikiongozwa na mkongwe Suleiman Ndikumana anayechezea
Inter Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, Burundi iliichapa Somalia mabao 5-1 jana
katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Tusker Challenge.
Katika mchezo
huo uliofanyika Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, mabao ya Burundi
yalifungwa na Chris Nduwarugira dakika ya 35 na 88, Yussuf Ndikumana dakika ya
41 na Suleiman Ndikumana dakika ya 84 na 90, wakati la Somalia lilifungwa na
Mohamed Jabril kwa penalti dakika ya 55.