Abdi Kassim 'Babbi' |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Salum Bausi Nassor amesema kwamba
amemtema katika timu hiyo, kiungo mkongwe Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ kwa
sababu ameongezeka uzito na amekuwa mzito sana.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana Uwanja wa Mandela, Namboole, Bausi alisema kwamba Babbi
anatakiwa kupambana na uzito ili arejeshwe Zanzibar Heroes.
“Kama
unavyoona, haya mashindano yamekuwa ya kasi sana sasa, na Babbi amekuwa mzito
sana na hata huko Azam, anaingizwa dakika 20 za mwisho, lazima uwe na wachezaji
wenye kasi, wewe mwenyewe umeona mechi na Eritrea ilivyokuwa ngumu,”alisema.
Awali ya
hapo, jana kipa namba moja wa Uganda Abbel Dhaira alisema kwamba anavutiwa sana
na uchezaji wa Babbi pamoja na wachezaji wengine, Mrisho Ngassa wa Tanzania
Bara na Haruna Niyonzima wa Rwanda.
“Hao ni
wachezaji ambao napenda sana kuwatazama, nasikia Babbi hajaja, sijui kwa nini,
kocha wao anajua, ila yule mchezaji mzuri sana, anapiga sana mashuti, ana
nguvu, ananivutia, namjua vema,”alisema Dhaira.
Zanzibar
juzi ilianza kwa sare michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Tusker Challenge inayoendelea mjini hapa, baada ya kutoka 0-0 na Eritrea
katika mchezo wa Kundi C.
Matokeo hayo
yanawaweka katika wakati mgumu kuweza kuendelea na mashindano haya na sasa
wanatakiwa kupambana zaidi katika mechi zao mbili zijazo ili washinde na
kutinga Robo Fainali.
Nahodha wa
Heroes, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ pamoja na kuwaomba radhi Wazanzibari kwa
sare hiyo, lakini pia ameahidi watajituma na kufanya vizuri katika mechi
zijazo.