Abbel Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KIPA namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira anayedakia klabu ya I.B.V FC ya Iceland, amesema
kwamba yuko tayari kuhama Ulaya na kuja Tanzania kuchezea klabu ya Simba, iwapo
watafika dau lake.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Dhaira alisema
kwamba mwaka jana Simba walimfuata, lakini wakashindwa kumalizana naye na
akaendelea kucheza Ulaya.
Hata hivyo,
Dhaira ambaye ni miongoni mwa makipa bora katika ukanda huu kwa sasa, alisema
anawapa nafasi nyingine Wekundu hao wa Msimbazi.
“Nina siku
tatu tu kabla ya kumaliza mkataba wangu na klabu yangu. Kabla ya kuingia nao
mkataba mpya, nawapa nafasi nyingine Simba SC,”alisema, Dhaira ambaye aliibukia
Express ya hapa mwaka 2006 kabla ya 2008 kuhamia U.R.A. pia ya hapa, ambayo
aliichezea hadi 2010 alipohamia Ulaya.
Hata hivyo,
Dhaira hataonekana tena kwenye michuano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya
Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuumia jicho katika
mechi ya kwanza dhidi ya Kenya, Jumamosi.
Akilizungumzia
hilo, Dhaira alisema imemsononesha sana kwani alijitoa kwa ajili ya kuja
kuisaidia nchi yake kwenye mashindano haya, lakini kwa bahati mbaya ameumia.
“Ni mambo ya
kawaida katika mchezo, nashukuru timu yetu ni nzuri na kuna wachezaji wengine
wazuri na ndiyo maana imeendelea kufanya vizuri,”alisema.
Simba SC kwa
sasa inasaka kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza, Juma Kaseja
ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo inafuatia makipa
wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha uwezo wa kumsaidia
Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili katika
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.