Kim Poulsen kushoto akiwa kocha wa vijana, Mdenmark mwenzake, Jacob Michelsen |
Na Princess Asia, Mwanza
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars,
Mdenmark Kim Paulsen amemuorodhesha kipa Juma Kaseja katika kikosi cha wachezaji
22 watakaounda kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars kitakachomenyana na Kenya, Harambee
Stars katika mchezo wa kirafiki ulio katika kalenda ya FIFA (Shirikisho la Soka
la Kimataifa) Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wiki ijayo.
Mbali na Kaseja wa Simba, Kim aliyepandishwa kutoka timu ya
vijana mwaka huu akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Borge Poulsen amemuita
pia kipa Deogratius Mushi wa Azam FC.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Mwanza leo, Paulsen
aliwataja wachezaji wengine ni mabeki Kevin Yondan wa Yanga, Aggrey Morris,
Erasto Nyoni wa Azam FC, Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe
na Amir Maftah wa Simba, wakati viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC,
Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa wa
Simba, Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo wa Yanga na Shaaban Nditi wa Mtibwa
Sugar.
Washambuliaji walioitwa na Paulsen ni John Bocco ‘Adebayor’ wa
Azam FC, Simon Msuva wa Yanga, Christopher Edward wa Simba, Mbwana Samatta na
Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
Tofauti na ilivyotarajiwa na wengi, Poulsen hajamuita mshambuliaji Jerry Tegete wa Yanga, ambaye ameonekana kufufua makali yake siku za karibuni.
Hata hivyo, Poulsen hakuchukua wachezaji wengi wa Zanzibar kwa
sababu nao watakwenda kujiunga na timu ya Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya
Kombe la CECAFA Tusker Challenge mwishoni mwa mwezi huu mjini Kampala, Uganda. Alisema
hicho ndio kikosi anachotarajia kukutumia katika Challenge. Kambi ya timu hiyo
itakuwa mjini Mwanza, kwa kuwa ni jirani na Uganda.