Wachezaji wa Serengeti Boys wakiomba dua kabla ya mazoezi yao Alhamisi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mungu ibariki Tanzania. Amin. |
Na Mahmoud Zubeiry
TIMU ya ya
taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, leo inashuka dimbani
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na vijana wenzao, Kongo
Brazzaville katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Tatu nay a mwisho ya mchujo
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Vijana chini ya umri wa miaka 17 nchini
Morocco mwakani.
Serengeti wanaingia
kwenye mchezo huo, wakiwa na matumaini makubwa ya ushindi kutokana na
maandalizi mazuri waliyopewa.
Kocha Mkuu
wa Serengeti Boys, Mdenmark Jacob Michelsen amesema ana matumaini ya ushindi
katika mchezo huo kutokana na maandalizi mazuri, ingawa amesema anaa wasiwasi
wapinzani wake wana wachezaji waliozidi umri.
Michelsen
alisema kwamba alikwenda kushuhudia mchezo wa kwanza wa raundi iliyopita, baina
ya Kongo na Zimbabwe waliotolewa na wapinzani wao hao na kujionea makali ya
wapinzani wao.
Pamoja na
kukiri kwamba Kongo ni timu bora na ilicheza Fainali zilizopita za Kombe la
Dunia nchini Mexico mwaka jana na kutolewa raundi ya pili, Michelsen alisema
bado ana wasiwasi timu hiyo ina ‘vijeba’.
“Nilipokwenda
kuwaangalia wakicheza na Zimbabwe, nilikuta kikosini mwao kuna wachezaji sita
wa kikosi kilichokwenda Mexico kwenye Kombe la Dunia, inanitia shaka kwa sababu
hakuna mchezaji anayeweza kucheza michuano mikubwa kama ile akiwa ana umri wa
miaka 15.
Mimi ni
kocha wa vijana na ninajua, haiwezekani. Ucheze fainali za Kombe la Dunia za
U17 una miaka 15, hakuna,”alisema Michelsen, ambaye aliwataja baadhi ya
wachezaji anaowatilia shaka wamezidi umri ni Hady Binguila na Charvely Mabiat.
Amesema
wamecheza mechi za kujipima nguvu 15 zikiwemo dhidi ya timu za Ligi Kuu na
hawajafungwa hata moja, kitu ambacho anaamini ni kipimo cha ubora wa timu yake.
Nahodha wa Serengeti
Boys, Miraj Adam amesema leoo watapigana kwa nguvu zao zote, kuhakikisha
wanawafunga Kongo Brazzaville ili watimize ndoto zao za kucheza Fainali za Morocco
mwakani.
Adam alisema
kwamba hata kama Kongo Brazzaville wamekuja na wachezaji waliovuka umri kwa
mujibu wa kanuni za mashindano hayo, lakini kesho watafungwa tu.
“Kongo
watakufa, watake wasitake, nasema Kongo watakufa,”alisema.
Kwa upande
wake, Msaidizi wake, Hussein Twaha ‘Messi’ alikumbushia maneno waliyoambiwa na
mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele katika ziara yake nchini hivi
karibuni na kusema yatakuwa kichocheo kwao kufanya vizuri na kukata tiketi ya
Morocco.
“Pele
alituambia mpira unachezwa na watoto kutoka familia masikini, hata yeye alitoka
familia ya kimasikini, akajitahidi akafanikiwa na kufanya watoto wake waingie
katika mpira wakitokea familia ya kitajiri, hivyo na sisi tunatumia kauli hii
kama kichocheo cha kufanya vizuri ili tufuate nyayo zake,”alisema Twaha.
Serengeti
imefanikiwa kufuzu hadi Raundi ya Tatu bila jasho, baada ya wapinzani wake wa
awali katika Raundi ya Kwanza na ya Pili, Kenya na Misri kujitoa. Iwapo timu
hii itafuzu, hii itakuwa mara ya pili kwa Serengeti kukata tiketi ya kucheza
fainali hizo, baada ya mwaka 2005.
Hata hivyo,
pamoja na kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, Serengeti haikwenda Gambia mwaka
huo kutokana na kuondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika
(CAF), baada ya kubainika walitumia kijana aliyezidi umri, Nurdin Bakari.