Aggrey Morris |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad
na Aggrey Morris sasa watabaki historia katika klabu ya Azam FC, kufuatia msimamo
wa Menejimenti ya timu hiyo, kuwafukuza moja kwa moja baada ya kuwakuta na
tuhuma za kuhujumu timu hiyo.
Wachezaji hao, wakiongozwa na Nahodha wao, Morris inadaiwa walipokea
rushwa kutoka kwa kiongozi wa juu kabisa wa klabu ya Simba, ambaye ukitajiwa
huwezi kuamini ili kuihujumu timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Aggrey aliondolewa kambini jana, siku moja tu baada ya kipa
Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Said Mourad na Erasto Nyoni nao kusimamishwa kwa
tuhuma hizo.
Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu na baada ya hapo ikamfukuza kocha wake
Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata
taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi kwa kushirikisha hadi na Taasisi ya
kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo imekamilisha uchunguzi na
ripoti imewataja wachezaji hao wanne kupokea rushwa kutoka kwa bosi huyo wa
Simba.
Hata hivyo, Dida hakucheza mechi hiyo, kwani Oktoba 27,
kikosi cha Azam kilikuwa;
Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris,
Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha
Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre
Herman Tcheche na Salum Abubakar.
Siku hiyo,
Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka
beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba
Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa
krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi
aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni
mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na
dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini
mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka
mabeki wa Azam.
Azam ambayo
leo inamenyana na Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kutokana na uhaba
wa mabeki wa kati, italazimika kutumia mabeki wa pembeni katikati leo ambao ni
Luckson Kakolaki na Samir Hajji Nuhu kuziba mapengo ya Mourad na Morris. Aidha,
katika beki ya kulia atacheza kiungo mshambuliaji, Kipre Balou.