Humphrey Mieno |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MCHEZAJI
mpya wa Azam, Humphrey Mieno jana alionyesha uwezo mkubwa katika mechi ya Kundi
A, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi
ya Uganda kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, mjini hapa.
Akicheza
kama kiungo mshambuliaji, Mieno alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira
kutulia nao, kutoa pasi na kuwazidi nguvu wachezaji wa timu pinzani katika
kugombea mipira, haswa ya juu.
Mieno ambaye
ni mrefu, alikuwa akiipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Uganda ambayo
ililazimika kumchunga mno.
Ana akili
sana ya mchezo- na wakati wote yupo mchezoni na jana mara mbili alikaribia
kufunga kama si jitihada za kipa Abel Dhaira, ambaye baadaye alitoka kufuatia
kuumia.
Mieno anayechezea
Sofapaka ya Kenya, ni kati ya wachezaji watatu walio mbioni kusajiliwa na Azam
kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la
Shirikisho la soka Afrika (CAF).
Wengine ni Eugene
Asike kutoka Sofapaka pia na Serge Wawa Paschal raia wa Ivory Coast anayechezea
El Merreikh ya Sudan. Azam FC imepania kuboresha kikosi chake katika dirisha
dogo, baada ya kufukuza wachezaji wanne mwishoni mwa mzuynguko wa kwanza wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa tuhuma za kuhujumu timu hiyo.
Wachezaji
hao ni kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Said
Mourad, wanaodaiwa kufanya hujuma katika mechi dhidi ya Simba, Oktoba 27, mwaka
huu.
Azam
imekwishasema imelifikisha suala hilo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kwa ajili ya hatua zaidi ili kukomesha desturi hiyo.
Wakati Azam
ikiwa katika mpango wa kusajili wachezaji watatu wapya wa kigeni, tayari
kikosini ina wachezaji wanne wa kigeni, ambao ni mabeki Mkenya Ibrahim
Shikanda, Mganda Joseph Owino na viungo washambuliaji Kipre Michael Balou na
Kipre Herman Tcheche kutoka Ivory Coast.
Kwa sababu
hiyo, Azam itatakiwa kupunguza wachezaji wawili katika wageni wake wa sasa ili
ibaki na wageni watano kulingana na kanuni za Ligi Kuu. Tayari Azam wako katika
mpango wa kumuhamishia Simba SC, Owino.
Azam pia
mbali na wachezaji wa kigeni, imejipanga kusajili wachezaji wakali wa nyumbani,
waliong’ara katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ili kuimarisha zaidi kikosi
chake.