Kazimoto |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
WACHEZAJI wawili
wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, beki Shomary Kapombe na kiungo Mwinyi
Kazimoto, walishindwa kumaliza mechi za jana, baada ya kuumia na sasa wako
hatarini kuikosa mechi ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Somalia, Desemba 1.
Wachezaji
hao wa klabu ya Simba, wote waliumia kipindi cha pili na kutolewa, nafasi ya
Kapombe ikichukuliwa na Issa Rashid wa Mtibwa Sugar nay a Mwinyi ikichukuliwa
na Shaaban Nditi wa Mtibwa pia.
Wote
walitoka wakichechemea, kuashiria wamepata maumivu makali kidogo na Kocha Mkuu
wa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen alisema ataangalia hali zao leo na kesho.
Kim pia
alisema kwamba sasa imetosha kuzungumzia suala la washambuliaji Mbwana Samatta
na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
kama watajiunga na timu hiyo au la.
“Kwangu sasa
lazima ifikie wakati iwe inatosha, sitaki kuwazungumzia tena wachezaji hao,
waulizeni TFF,”alisema Poulsen baada ya kuulizwa kama mawasiliano na klabu yao
kama yanaendelea juu ya kuombea ruhusa.
Mazembe
imekataa kuwaruhusu wachezaji hao kwa sababu michuano ya Challenge haimo kwenye
kalenda ya FIFA.
Kutokana na
kukosekana kwa washambuliaji hao, Stars sasa inabaki na mshambuliaji mmoja tu
kikosini, John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC, ambaye Watanzania wanatakiwa
kumuombea dua asiumie ili aendelee kuibeba timu yao ya taifa.