Yanga SC |
Na Mahmoud Zubeiry
UHONDO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatarajiwa
kuendelea leo, ‘Big Three’ zikijitupa uwanjani kuwania pointi za kutengeneza
mazingira ya ubingwa mskmu huu.
Mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wakati washindi wa pili wa ligi hiyo
msimu uliopita, Azam FC watakuwa wanaonyeshana kazi na washindi wa tatu, Yanga
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kweli hata mchezo wa Morogoro utavuta hisia za wengi, lakini
mchezo mkali zaidi na uliobeba zaidi mustakabali wa msimamo wa Ligi Kuu utakuwa
Dar es Salaam.
Yanga na Azam FC kwa sasa ni wapinzani wakubwa- na hapana
shaka Watoto wa Jangwani sasa wanaamini uzito wa mechi dhidi ya Wana Lamba
Lamba ni sawa na uzito wa mechi dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC.
Na bila shaka ni kwa sababu hiyo, baada ya mechi yao na
Mgambo JKT Yanga wakaenda kuweka kambi katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani
Pwani kujiandaa na mchezo wa leo.
Kwa kawaida, Yanga huweka kambi Bagamoyo katikati ya Ligi,
inapokuwa inajiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC hivyo
kwa kwenda huko kuweka kujiandaa na mchezo huo, maana yake wanaupa uzito sawa
na pambano la watani.
Wakati vijana wa Yanga wakiwa Bagamoyo, Kocha Mkuu wa klabu
hiyo, Mholanzi Ernie Brandts Alhamisi alikwenda kwenye Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, kuifuatilia timu hiyo ilipokuwa ikimenyana na Coastal Union ya Tanga.
Katika mchezo huo, Brandts aliyeambatana na Msaidizi wake,
Freddy Felix Minziro alikuwa makini kufuatilia uchezaji wa Azam na kunukuu
kwenye kijitabu chake, maana yake alikwenda kufanyia kazi katika mazoezi ya
timu yake.
Azam nayo, ina ari mpya baada ya kurejea kwa kocha wake
Muingereza, Stewart Hall aliyewapa mafanikio makubwa uliopita.
Stewart amerejea na ‘bonge la zali’ Azam, baada ya kuiongoza
timu hiyo kuichapa Coastal mabao 4-1 siku hiyo, ikitoka kuchapwa mabao 3-1 na
Simba SC, chini ya kocha aliyefukuzwa baada ya mechi hiyo, Mserbia, Boris
Bunjak.
Stewart alifukuzwa Azam Agosti mwaka huu, baada ya kikiuka
maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu, kwa kumpanga Mrisho Ngassa katika
Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga. Yanga
ilishinda 2-1 na kutwaa Kombe.
Lakini amerejeshwa kufuatia wachezaji wa Azam kuuandikia
barua uongozi ya kumkataa Bunjak na kupendekeza Muingereza huyo arejeshwe. Na
uongozi wa Azam pia ulizingatia kushuka kwa kiwango cha timu na kukubaliana na
pendekezo la wachezaji wake.
Azam itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 4-1,
uliowafanya wafikisha pointi 21, baada ya kucheza mechi 10 na kurejea nafasi ya
tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Simba na Yanga, zenye pointi 23 zote
baada ya kucheza mechi 11, kila timu.
Yanga SC nao watashusha timu yao wakiwa na kumbukumbu ya wimbi
la ushindi katika Ligi Kuu ikiwemo mechi ya iliyopita, ambayo waliichapa Mgambo
JKT ya Handeni, Tanga mabao 3-0 Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na kuifikia kwa pointi Simba SC iliyotoa sare ya 1-1 na Polisi mjini Morogoro siku
hiyo.
Faraja kwa Yanga ni kurejea kwa wachezaji wake tegemeo, beki
Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi ‘Spider Man’, ambao walikuwa
majeruhi. Yondan aliingia kipindi cha pili katika mechi dhidi ya Mgambo, wakati
Bahanuzi alipewa mapumziko zaidi, ingawa leo anaweza kupangwa.
Kwa Azam nako, faraja yao mbali na kurejea kwa Stewart, pia
ni kurudi kwa mpachika mabao wao tegemeo,
John Bocco ‘Adebayor’ aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.
Wakati Brandts akionyesha kutilia mkazo mechi hiyo kiasi cha
kwenda hadi Chamazi kushuhudia mbinu za wapinzani wake, Stewart naye alisema
baada ya mechi ya Coastal wanataka kuwafunga Yanga leo.
Katika mchezo wa leo, bila shaka Stewart hatafanya mabadiliko
makubwa kutoka kikosi kilichotandika Coastal 4-1.
Langoni anaweza kuendelea kusimama Mwadini Ally, kulia Samir
Hajji, kushoto Ibrahim Shikanda, katikati Aggrey Morris na Said Mourad katika
safu ya ulinzi, Jabir Aziz kiungo mkabaji, viungo wa pembeni Kipre Balou na
Khamis Mcha ‘Vialli’, kiungo mchezeshaji Salum Abubakar na washambuliaji John
Bocco na Kipre Tcheche.
Brandts pia hatarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa kwenye
kikosi chake leo, kutoka kile kilichoichapa 3-0 Mgambo JKT.
Utata tu utakuwa baada ya kurejea Yondan, Mbuyu Twite
atampanga pembeni au ataamua kumuanzishia benchi mmoja kati ya mabeki wake
watatu wa kati, mwingine akiwa ni Nadir Haroub Cannavaro.
Leo bila shaka Yawe Berko atadaka badala ya Ally Mustafa
‘Barthez’ na kama Twite ataanzishwa kulia, maana yake Nahodha Nsajigwa Shadrack
atapumzika, kushoto Oscar Joshua, katikati
wawili kati ya Twite, Cannavaro na Yondan, kiungo mkabaji Athumani Iddi
‘Chuji’, viungo wa pembeni Simon Msuva na Hamisi Kiiza, kiungo mchezeshaji
Haruna Niyonzima na washambuliaji Said Bahanuzi na Didier Kavumbangu.
Lakini katika mechi za karibuni, Brandts amekuwa akitumia
viungo wawili wakabaji na mshambuliaji mmoja, ili kumfanya Niyonzima acheze
zaidi na Frank Domayo ndiye amekuwa akichukua nafasi ya mshambuliaji.
Haijulikani katika mchezo wa leo kama Mholanzi huyo
ataendelea na mbinu hiyo hiyo au ataamua kutumbukiza washambuliaji wawili.
Mara ya mwisho Yanga na Azam zilikutana katika fainali ya
Kombe la Kagame, Agosti 10, mwaka huu na Watoto wa Jangwani wakaibuka vinara na
kutwaa Kombe kwa ushindi wa 2-1.
Mjini Morogoro nako, nyasi za Uwanja wa Jamhuri zitahimilii
vishindo vya Simba na Mtibwa, ambao katika miaka ya karibuni, wamekuwa vibonde
wa Wekundu hao wa Msimbazi.
Simba iliendelea kubaki mkoani Morogoro, baada ya sare ya 1-1
na Polisi Jumatano, kujiandaa na mchezo wa leo, ikiwa imeweka kambi maeneo ya
Nane Nane mkoani humo, huku ikijifua kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Wekundu hao wa Msimbazi, wamepania kushinda mechi ya kwanza
nje ya Dar es Salaam leo, baada ya awali kutoa sare katika mechi zake zote za
ugenini.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba ilitoka sare za bila
kufungana na wenyeji Coastal Union na Mgambo JKT kabla ya juzi kufungana 1-1 na
Polisi, tena yenyewe ndio ikihaha hadi kipindi cha pili kukomboa bao, baada ya
Mokili Rambo kutangulia kuwafungia Maafande hao kipindi cha kwanza.
Mkombozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, alikuwa ni kiungo Amri
Kiemba juzi, ambaye hilo linakuwa bao lake la tano msimu huu.
Pamoja na hayo, Simba inajivunia kuwa timu pekee ambayo hadi
sasa haijapoteza mechi hata moja katika Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa
pointi zake 23 sawa na Yanga, baada ya kucheza mechi 11, lakini ina wastani
mzuri zaidi wa mabao.
Zaidi ya sare hizo tatu, Simba ilitoa sare nyingine mbili
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba 2-2 na Yanga
SC, wapinzani wao wa jadi, 1-1.
Azam FC |
REKODI YA YANGA AZAM
FC:
Machi 10, 2012
Yanga 1 – 3 Azam
Septemba 18, 2011
Azam 1 – 0 Yanga
Machi 30, 2011
Yanga 2-1 Azam
Oktoba 24, 2010
Azam 0-0 Yanga
Machi 7, 2010
Yanga 2-1 Azam
Oktoba 17, 2009
Azam 1-1 Yanga
Aprili 8, 2009
Yanga 2-3 Azam FC
Oktoba 15, 2008
Azam FC 1-3 Yanga
Simba SC |
REKODI YA SIMBA NA
MTIBWA TANGU 2005:
Machi 18, 2012
Simba 2 – 1 Mtibwa Sugar
Septemba 25, 2011
Simba 1 – 0 Mtibwa Sugar
Februari 27, 2011
Simba 4 – 1 Mtibwa Sugar
Feb 27, 2011
Simba 4-1 Mtibwa Sugar
Sept 29, 2010
Mtibwa Sugar 0-1 Simba
Machi 22, 2009
Mtibwa Sugar 1-0 Simba
Sep 28, 2010
Simba 1-0
Mtibwa Sugar
Apr 21, 2010
Mtibwa Sugar 0-4
Simba
Nov 15, 2009
Simba 3-1
Mtibwa Sugar
Feb 20, 2008
Simba 1-1
Mtibwa Sugar
Okt 7, 2007
Mtibwa Sugar 1-3
Simba
2007: Hazikukutana
kwenye Ligi ndogo
Sept 10, 2006
Mtibwa Sugar 1-1
Simba
Apr 9, 2006
Simba 1-1
Mtibwa Sugar
Okt 5, 2005
Simba 2-1
Mtibwa Sugar
Mei 22, 2005
Mtibwa Sugar 0-1
Simba
Mtibwa Sugar |