Kavumbangu |
Na Prince Akbar
KIUNGO
Rashid Gumbo na mshambuliaji Didier Kavumbangu ni wachezaji pekee wa Yanga,
ambao hawajaanza mazoezi baada ya mapumziko mafupi ya wiki mbili na hawana
sababu.
Habari kutoka
ndani ya Yanga, zimesema kwamba wachezaji wote ambao hawapo kwenye timu
zinazoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge wanaendelea na mazoezi Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es
Salaam kasoro watano.
Wachezaji ambao
hawapo mazoezini pamoja na Gumbo na Kavumbangu, ni mabeki Ladislasu Mbogo, David
Luhende na kiungo Shamte Ally.
Imeelezwa Shamte
na Luhende ni wagonjwa, wakati Mbogo amekwenda kumuuguza mama yake, Mwanza. “Gumbo
na Kavumbangu hawana sababu,”kilisema chanzo.
Gumbo amekuwa
akilalamikia kuwekwa benchi na kuna wakati alifikia pia kusema anataka kuondoka
kwenda timu ambayo atakuwa anacheza.
Kavumbangu yuko
kwenye mpango wa kuuzwa Qatar, lakini bado hiyo haiwezi kuhusiana na kutohudhuria
kwake mazoezi.
Yanga imepanga
kufanya ziara ya mafunzo nchini Uturuki mwishoni mwa Desemba na mwanzoni mwa Januari
mwakani, kabla ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame mjini Kigali, Rwanda.
Mabingwa hao
mara tano wa Kagame, 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, wamepania kutwaa ubingwa
wa Ligi Kuu msimu huu kurejesha heshima yao na wamewekeza kwenye maandalizi
mazuri kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.
Yanga ilimaliza
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza kwa pointi zake 29, ikifuatiwa
na Azam yenye 24, wakati mabingwa watetezi Simba SC wana pointi 23.