Daniel Akuffo kushoto akimfariji Kaseja Jumamosi mjini Morogoro. Kushoto kabisa na Haruna Chanongo |
Na Mahmoud Zubeiry
NAHODHA wa
Simba, Juma Kaseja kwa siku ya pili mfululizo leo hajafika kwenye mazoezi ya
timu yake inayojiandaa na mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, utakaopigwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
huku kukiwa kuna habari ameamua kuachana na timu hiyo.
Mazoezi ya Simba
yanaendelea kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam jioni hii, lakini
Kaseja hayupo na Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema wanaendelea
kumpa nafasi kwa kuwa wanafahamu yupo katika wakati mgumu kwa sasa, baada ya
fujo alizofanyiwa na mashabiki Jumamosi Morogoro.
Jana ilielezwa
kwamba Kaseja amewaaga wachezaji wenzake na kuwaambia yeye na klabu hiyo basi.
BIN ZUBEIRY ilifika kwenye mazoezi ya Simba
jioni ya jana Uwanja wa Kinesi na kukuta wachezaji wote wakiendelea na mazoezi
kujiandaa na mechi ya Toto, kasoro Kaseja na Amir Maftah.
Alipoulizwa
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kwamba Maftah ana ruhusa maalum
kwa sababu ameoa hivi karibuni, lakini Kaseja hawana taarifa zake, ila;
“Nadhani hatakuwa vizuri kisaikolojia baada ya kufanyiwa fujo Jumamosi,”alisema
Kamwaga.
Lakini BIN
ZUBEIRY ilipozungumza na wachezaji wenzake, walisema Nahodha wao
amewaaga kwamba yeye na Simba basi, kwani ameumia sana kwa jinsi alivyodhalilishwa
na mashabiki Jumamosi Morogoro.
“Juma hapa
ndio basi kaka, Kasema yeye na Simba basi, amesononeshwa mno na jinsi
alivyodhalilishwa baada ya mechi ya Morogoro,”alisema mchezaji mmoja wa Simba
baada ya mazoezi Kinesi leo.
Kaseja
alitukanwa na kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba baada ya mechi dhidi ya
Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakimtuhumu kufungwa mabao ya
kizembe.
Lakini
tayari uongozi wa Simba umelaani vikali vurugu na vitisho alivyotolewa kipa wao
huyo namba moja, na kusema wanafikiria
kuwachukulia hatua kali watu waliomfanyia hivyo Nahodha wao huyo.
Juhudi za
kumpata Kaseja mwenyewe kuzungumzia suala hilo, hazikuweza kufanikiwa kwani
simu yake ilikuwa haipatikani.