Kaseja akiomba dua katika moja ya mechi za timu hiyo |
Na Mahmoud Zubeiry
NAHODHA wa
Simba, Juma Kaseja kwa siku ya tatu mfululizo jana ameendelea na mgomo wake wa
mazoezi ya timu yake inayojiandaa na mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, utakaopigwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
huku kukiwa kuna habari ameamua kuachana na timu hiyo.
Lakini tofauti
na siku mbili za awali, Kaseja jana alifika kwenye Uwanja wa Kinesi, ila mtazamaji
kama watazamaji wengine.
Hakufanya mazoezi,
ingawa alipoulizwa alisema yeye bado bado mchezaji wa Simba na ana mkataba na
timu hiyo.
Mwanzoni mwa
wiki ilielezwa kwamba Kaseja amewaaga wachezaji wenzake na kuwaambia yeye na
klabu hiyo basi.
Hatua hiyo
ilifuatia Kaseja kutukanwa na kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba baada ya
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakimtuhumu
kufungwa mabao ya kizembe.
Lakini
tayari uongozi wa Simba umelaani vikali vurugu na vitisho alivyotolewa kipa wao
huyo namba moja, na kusema wanafikiria
kuwachukulia hatua kali watu waliomfanyia hivyo Nahodha wao huyo.