Kado |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA namba
moja wa Mtibwa Sugar, Shaaban Hassan Kado amepata ajali ya gari leo akiwa
anaelekea Morogoro, ambako timu yake inamenyana na Simba SC katika mchezo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo.
Kocha wa
Mtibwa Sugar, Mecky Mexime ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Kado alikuwa
anakwenda Morogoro kujiunga na wenzake kambini, akitokea nyumbani kwao Dar es Salaam.
Alipoulizwa kwa
nini kipa huyo hakuwa kambini wakati timu yake ina mechi leo, Mexime alisema; “Kado
anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, kwa hivyo hayuko kwenye programu ya mechi
ya leo. Alikuwa ana ruhusa fupi ya kwenda kwao,”alisema.
Mexime alisema
Kado alipata ajali kwanza kwa gari yake anaelekea Morogoro, na akaiacha na
kupanda gari kurudi Dar es Salaam na akiwa kwenye gari hilo lingine, kipa huyo
wa zamani wa Yanga alipata tena ajali.
“Baada ya
ajali hiyo mimi ndio nikamfuata kwenda kumchukua na sasa niko naye njiani
tunaelekea Morogoro moja kwa moja hospitali,”alisema.
Hata hivyo, Nahodha
huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars alisema Kado hajaumia
sana, amepata michubuko kidogo tu kichwani kutokana na kuchanwa na kioo cha gari
na zaidi anasema anasikia maumivu sehemu ya kiuononi.