Bocco kulia akitafuta mbinu za kumtoka Paschal Ochieng wa Simba katika mechi dhidi ya Simba. |
Na Mahmoud Zubeiry
MPACHIKA mabao tegemeo wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’
amepona maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata wiki iliyopita kwenye mechi
dhidi ya Simba Sc na jioni ya leo anatarajiwa kuanza mazoezi na wenzake, Uwanja
wa Azam Complex, Chamazi, kujiandaa na mechi ya Jumapili dhidi ya Yanga.
Bocco aliumia na kutoka uwanjani dakika ya 22 katika mchezo
huo, baada ya kuifungia Azam bao la kuongoza, kabla ya Simba kutoka nyuma na
kushinda 3-1.
Kocha Muingereza Stewart Hall amefurahia kurejea kwa Bocco
kikosini na anaami hilo ni ongezeko la matumaini ya ushindi Jumapili.
Stewart amerejea na ‘bonge la zali’ Azam, baada ya jana
kuiongoza timu hiyo kuichapa Coastal Union ya Tanga mabao 4-1 katika mchezo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Stewart alitua juzi usiku Dar es Salaam akitokea Kenya
alipokuwa anaifundisha Sofapaka ya Ligi Kuu ya huko, baada ya kufukuzwa Azam
Agosti mwaka huu na leo ameanza kazi, akirithi mikoba ya Mserbia, Boris Bunjak
aliyefukuzwa Jumatatu.
Kwa ushindi huo, Azam imefikisha pointi 21, baada ya kucheza
mechi 10 na sasa inarejea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya
Simba na Yanga, zenye pointi 23 zote baada ya kucheza mechi 11, kila timu.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Simon Mbelwa,
aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wote wa Pwani na Michael Mkongwa wa Njombe,
hadi mapumziko Azam tayari walikuwa wanaongoza kwa mabao 3-0.
Gaudence Mwaikimba aliifungia Azam bao la kwanza kwa kichwa
dakika ya 23 kabla ya Kipre Tcheche kufunga la pili dakika ya 36, baada ya
kuipasua ngome ya Coastal na Khamis Mcha ‘Vialli’ akafunga la tatu dakika ya
44.
Coatsal walianza vizuri mechi hiyo na kusukuma mashambulizi
langoni mwa Azam, lakini baada ya dakika 20, wakapoteza mwelekeo na kuanza
kuwaruhusu wapinzani wao kuvuna mabao.
Kipindi cha pil, Azam walirudi na moto wao, lakini kidogo
Coastal walibadlika nao na kufanya mchezo uwe mgumu kidogo.
Hata hivyo, walikuwa ni Azam tena waliotikisa nyavu za
Coastal, baada ya kiungo Othman Tamim kujifunga dakika ya 73 katika harakati za
kuokoa.
Baada ya bao hilo, Coastal walizinduka na kuanza kushambulia
kupitia pembeni, jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la kufutia machozi
lililofungwa ma kiungo Jerry Santo.
Kwa ujumla katika mchezo wa jana, Coastal walizidiwa katika
safu ya kiungo ambako Stewart alipanga viungo wengi waliotekeleza majukumu yao
vyema.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Coastal, Hemed Morocco alisema
kwamba walizidiwa uwezo na wapinzani wao na kwa ujumla vijana wake walicheza
chini ya kiwango jana, hata hivyo anakwenda kufanyia kazi makosa ili timu
irejeshe makali yake.
Stewart alisema anafurahi kukaribishwa na ushindi huo mnono
na kwamba hizo ni dalili njema. Aliwapongeza vijana wake kwa kucheza kwa
kufuata maelekezo yake na akasema kwamba sasa anaelekeza nguvu zake katika
mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam FC; Mwadini Ally, Samir Hajji, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris,
Said Mourad, Kipre Balou/Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Salum Abubakar/Himid
Mao, Gaudence Mwaikimba/Abdi Kassim, Kipre Tcheche na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Coastal Union; Jackson Chove, Said Swedi, Juma Jabu, Mbwana Hamisi, Jamal
Machelanga/Salim Gilla, Jerry Santo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Razack
Khalfan/Hamisi Shango, Daniel Lyanga, Atupele Green/Lameck Dayton na Othman
Tamim.